Jul 07, 2022 02:22 UTC
  • Uungaji mkono wa wanazuoni wa Bahrain kwa mpango wa Sheikh Isa Qassim; umoja wa wapinzani wa utawala wa Aal Khalifa

Kwa kuunga mkono taarifa iliyotolewa na Sheikh Isa Qassim, kiongozi wa kidini, dhidi ya utawala wa Aal Khalifa, wanazuoni wa Bahrain wamesisitiza udharura wa kuwepo umoja miongoni mwa wapinzani wa utawala wa kidikteta wa nchi hiyo.

Tangu Februari 2011 hadi sasa, Bahrain imekuwa ikishuhudia maandamano na mapambano ya wananchi dhidi ya utawala wa kidikteta wa nchi hiyo. Sheikh Isa Qassim, kiongozi wa kidini wa watu wa nchi hiyo amekuwa akiongoza mapambano hayo na hivi karibuni ametoa taarifa muhimu ambayo ina nukta kadhaa za kuzingatiwa.

Nukta ya kwanza ni kwamba mshindi wa mgawanyiko wowote unaoweza kutokea kati ya wanamapambano na wapinzani wa utawala wa kidikteta wa Bahrain ni watawala wa hivi sasa wa Manama. Kimsingi ni kuwa kila nchi inayokabiliwa na mgawanyiko wa watu wake wanaopambana dhidi ya utawala dhalimu na wa kidikteta, uwe ni mgawanyiko wa kidini, kisiasa au kijografia, bila shaka huwa ni kwa manufaa ya serikali iliyoko madarakani ambayo hutumia fursa hiyo kwa ajili ya kuwakandamiza zaidi watu wake na kuzidisha matatizo na mashaka yao.

Watawala wa Bahrain ni marafiki wakubwa wa Wazayuni ambao ni maadui wakubwa wa Waislamu na Waarabu

Nukta nyingine ni kwamba taarifa hiyo inazungumzia udharura wa kulindwa heshima na utukufu wa mwanadamu kwa kutilia maanani kwamba mfarakano kati ya wapinzani ni fursa nzuri kwa ajili ya utawala kulinda na kudumisha hali iliyopo au hata kuharibu zaidi hali ya mambo kwa madhara ya taifa zima.

Nukta nyingine iliyotiliwa maanani katika taarifa hiyo ya Sheikh Isa Qassim ni kwamba utawala wa kidikteta daima hulenga umoja na mshikamano uliopo kati ya viongozi wa upinzani. Umoja huo ni moja ya nguzo muhimu zinazopelekea ushindi wa mapambano ya wananchi na bila shaka matokeo ya mifarakano na utengano miongoni mwa viongozi wa upinzani ni ushindi kwa utawala wa kidikteta.

Stratijia muhimu ambayo imekuwa ikifuatwa na utawala wa kidikteta wa Aal Khalifa kwa miaka 11 iliyopita ni kukabiliana na mapambano ya watu wa Bahrain na kuzidisha hitilafu katika safu za wapinzani. Kwa ibara nyingine ni kwamba watawala wa Bahrain wamekuwa wakitekeleza siasa kongwe za mabwana zao wa Uingereza za kutenganisha watu kwa ajili ya kupata fursa ya kuwatawala. Katika uwanja huo, watawala wa Aal Khalifa kwa uungaji mkono wa vyombo vya habari vya serikali pamoja na vya baadhi ya serikali za eneo na hasa ya Saudi Arabia, vimejaribu kuonyesha, kinyume na ukweli wa mambo kuwa, mapambano halali ya Wabahraini ni mapambano ya Mashia dhidi ya Masuni.

Hoja inayotolewa na watawala wa Manama kuhusu fitina hiyo ni kwamba kwa kutilia maanani ukweli kuwa Mashia ndio wengi nchini Bahrain, hivyo wanafanya kila juhudi ili kupata fursa ya kutawala nchini humo. Madai hayo yanatolewa katika hali ambayo mapambano ya watu wa Bahrain hayana utambulisho wowote wa kimadhehebu wala kidini bali yanataka kuundwa utawala wa kiadilifu na wa kidemokrasiua ambao utazingatia kwa usawa matakwa ya wananchi wote wa nchi hiyo bila kuwabagua kwa misingi ya kiukoo na kimadhebeu. Ni wazi kuwa viongozi na washiriki wa mapambano hayo ni kutoka madhehebu zote mbili za Shia na Suni.

Ni siasa hizo za kuibua fitina za kimadhehebu ndizo zimepelekea kufanikiwa kwa kiwango fulani njama za viongozi wa Manama za kudhoofisha na kupunguza kasi ya mapambano na maandamano ya wapinzani dhidi ya utawala wao. Suala hilo limezingatiwa pia katika taarifa ya Sheikh Isa Qassim ambaye amewasihi Wabahrain kujiepusha na mifarakano na fitina ambazo huenda zikawadhuru zaidi na kuwafanya waendelee kuishi kwenye umasikini na udhalili unaochochewa na watawala wa Aal Khalifa dhidi yao.

Askari wa kigeni wanaolinda utawala wa Bahrain unaoendelea kukandamiza watu wake

Taarifa hiyo ya Sheikh Isa Qassim imepokelewa vizuri na wanazuoni wengi wa Bahrain. Baadhi ya maulama wa Bahrain ambao wanashikiliwa na utawala wa Manama wametoa taarifa ya pamoja wakiyataka makundi ya upinzani kushirikiana kwa ajili ya kuimarisha umoja kati yao.

Wanazuoni hao pia wamesisitiza nukta mbili muhimu. Ya kwanza ni kuwa hakuna maendeleo yoyote yanayoweza kufikiwa bila ya kuwepo umoja na pili ni kwamba mafundisho ya dini na uzoefu wa wanadamu unathibitisha wazi kuwa mifarakano na migawanyiko hatimaye huleta udhaifu, kushindwa na kuendelea kutawala dhulma na uonevu.

Hata kama utawala wa Aal Khalifa unasaidiwa na kuungwa mkono na tawala za Saudi Arabia, Israel na Marekani lakini bila shaka umoja miongoni mwa Wabaharaini na wapinzani wa utawala wa kidikteta wa Manama uneweza kudhoofisha na hatimaye kuvunja nguzo za utawala huo wa kibaraka.

Tags