Jul 07, 2022 11:24 UTC
  • Rais wa Lebanon: Karibu tutafikia mwafaka na Israel juu ya uainishaji mipaka ya baharini

Rais Michel Aoun wa Lebanon ametangaza kuwa, karibuni hivi suala la uanishaji mipaka ya baharini baina ya nchi hiyo na utawala wa Kizayuni wa Israel litapatiwa ufumbuzi na kwamba njia hiyo ya utatuzi wa mzozo huo itaridhiwa na pande zote.

Toleo la leo la gazeti la Ra'ayul-Yaum limeripoti kuwa rais Aoun amesema, kutatuliwa suala la uainishaji mipaka ya baharini ni kwa manufaa ya pande zote; na katika kadhia kama hiyo inapasa pande zote mbili ziridhike na njia ya utatuzi iliyopendekezwa; vyenginevyo hatua yoyote itakayochukuliwa itakuwa sawa na uchokozi na uvamizi.

Rais wa Lebanon ameongezea kwa kusema: "ninaamini tunakaribia kufikia maelewano na Marekani, ambayo ndiye mpatanishi baina ya Lebanon na utawala wa Kizayuni; ni kwa sababu kuna anga chanya katika suala hili, kwani kama isingekuwa hivyo, ingepasa tusitishe mazungumzo".

Aoun amesisitiza kuwa njia ya ufumbuzi iliyoafikiwa ndio msimamo rasmi kwa nchi nzima ya Lebanon. 

Awali duru moja rasmi ya Lebanon ilitangaza kuwa, serikali ya Beirut imeitaka Marekani iulazimishe utawala wa Kizayuni wa Israel usimamishe harakati zozote unazofanya katika eneo la bahari linalozozaniwa na utawala huo na Lebanon.../

 

Tags