Jul 09, 2022 07:35 UTC
  • Makundi ya muqawama Palestina yamkosoa Abbas kukutana na Gantz

Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina Mahmoud Abbas amekosolewa vikali na makundi ya muqawama ya Palestina, kwa kukutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Vita wa utawala wa Kizayuni wa Israel, Benny Gantz.

Msemaji wa Harakati ya Muqawama ya Jihadul Islami, Tariq Salmi amesema mkutano huo wa Abbas na Benny Gantz, Waziri wa Vita wa Israel hautakuwa na matokeo mengine ghairi ya kushadidisha migawanyiko ya kisiasa miongoni mwa Wapalestina.

Naye, Hazem Qassem, Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema kitendo cha Abbas kwenda kujikomba mbele ya Waziri wa Vita wa Israel ni sawa na kuipiga jambia kwa nyuma kambi ya Inifadha.

Abbas na Gantz walikutana na kufanya mazungumzo katika kikao cha faragha jioni ya juzi Alkhamisi mjini Ramallah, katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Wawili huo walijadili mikakati ya usalama kuelekea safari ya Rais Joe Biden wa Marekani katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu baina ya Julai 13 na 16.

Nembo za kambi ya muqawama

Abbas anaendelea kujikomba kwa Wazayuni katika hali ambayo, Naftali Bennett, Waziri Mkuu aliyeondoka wa utawala khabithi wa Israel mwenye misimamo ya kufurutu ada amesisitiza mara kadhaa kuwa, kamwe hatoruhusu kuundwa dola la Palestina katika utawala wake.

Abbas jana Ijumaa pia alizungumza kwa njia ya simu na Yair Lapid, Waziri Mkuu mpya wa utawala wa Kizayuni wa Israel, hii ikiwa mara ya kwanza baada ya miaka mingi kwa kiongozi huyo wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina kufanya mazungumzo na waziri mkuu wa Israel.

Tags