Jul 16, 2022 02:42 UTC
  • Shukurani za Gavana wa jimbo la Herat kwa misaada ya Iran kwa  watu wa Afghanistan

Gavana wa jimbo la Herat ameishukuru Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa misaada yake kwa watu wa Afghanistan.

Maulana Nur Ahmad Jar, ametoa shukurani hizo katika mazungumzo na Mohammad Seddiqi Far, mkuu wa ubalozi mdogo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika jimbo hilo la magharibi ya Afghanistan. 

Mbali na kuishukuru Iran kwa misaada inayowapatia wananchi wa Afghanistan, Gavana wa Herat ameomba uanzishwe tena utaratibu wa utoaji viza za kazi nchini Iran kwa raia wa Afghanistan.

Katika mazungumzo hayo Ahmad Jar ametaka pia kustawishwa uhusiano wa pande mbili kati ya Iran na Afghanistan katika nyuga mbalimbali.

Mohammad Seddiqi Far (kushoto) na  Maulana Nur Ahmad Jar

Kwa upande wake, Mohammad Seddiqi Far, mkuu wa ubalozi mdogo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Herat amesema, viongozi wa Iran wako tayari kupanua zaidi mashirikianano na serikali ya Afghanistan katika nyanja zote na akaongezea kwa kusema: "suala la viza ya kazi litawasilishwa kwa maafisa waandamizi wa Jamhuri ya Kiislamu; na hivi sasa yanafanyika mashirikiano kwa ajili ya kutekeleza mchakato huu".

Msaada wa Iran kwa Afghanistan inaotoa kwa kupeleka misaada ya kibinadamu nchini humo au kwa kuwapokea wakimbizi na wahajiri wa Kiafghani, ndio masuala muhimu zaidi yaliyogusa uhusiano baina ya nchi hizi mbili kwa miongo kadhaa sasa.

Tangu Taliban iliposhika tena hatamu za utawala nchini Afghanistan mwezi Agosti mwaka uliopita, hadi kufikia sasa ambapo nchi hiyo imekuwa ikikabiliwa na mgogoro mkubwa wa kiuchumi unaotokana na msimamo wa jamii ya kimataifa wa kutokuwa tayari kulitambua rasmi kundi hilo wala kuonyesha hamu ya kushirikiana na Afghanistan, hali za maisha ya watu zimezidi kuwa mbaya.

Viongozi wa Taliban

Kukosekana fedha zinazohitajika kwa ajili ya kuagizia bidhaa muhimu kama mchele, shairi, ngano na mahindi, ambako kumesababisha uhaba na ughali wa bidhaa za chakula kwenye masoko ya ndani, kumehatarisha usalama wa chakula nchini Afghanistan; na asasi za haki za binadamu tayari zimeshatoa indhari kuhusu hali mbaya ya maafa ya kibinadamu yanayotokana na njaa na ukame yatakayowakumba mamilioni ya watu nchini humo.

David Beasley, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani WFP anasema:

Kwa uchache, karibu nusu ya watu wote nchini Afghanistan wanakabiliwa na baa la njaa. Watu Afghanistan wanahitaji misaada ya haraka ya kibinadamu; na iwapo misaada hiyo haitapatikana, Afghanistan itageuka eneo la maafa makubwa ya kibinadamu".

David Beasley

Wakati Afghanistan inakabiliwa na hali mbaya ya kushindwa kujidhaminia mahitaji yake ya chakula, dawa na huduma za afya, Iran, kama ilivyofanya katika miongo kadhaa iliyopita kwa kuwa pamoja muda wote na watu wa nchi hiyo kwa shida na raha, hadi sasa imepeleka mara kadhaa misaada mbalimbali ya kibinadamu katika maeneo na majimbo tofauti ya Afghanistan katika kipindi cha tangu Taliban iliposhika tena madaraka. 

Na hasa katika wiki kadhaa zilizopita, ambapo kutokana na majanga ya mafuriko na tetemeko la ardhi yaliyotokea Afghanistan, misaada ya kibinadamu iliyopelekwa na Iran nchini humo imewaliwaza na kuwafariji wananchi wa Afghanistan waliokumbwa na majanga hayo ya kimaumbile wakikabiliwa pia na matatizo yanayotokana na mgogoro mkubwa wa kiuchumi na hali mbaya ya kimaisha inayotawala nchini humo.

Shukurani za Liwali wa mkoa wa Herat kwa Iran kutokana na misaada inayotoa kwa watu wa Afghanistan inabainisha jinsi viongozi wa kitaifa pamoja na wa mikoa wa serikali ya Taliban wanavyoelewa vyema jinsi Tehran inavyoyaangalia kwa jicho la ubinadamu matukio na hali ya nchi hiyo.

Shehena ya misaada ya kibinadamu ya Iran ikiwasili Afghanistan

Na hii ni katika hali ambayo, kuhusiana na mgogoro wa kiuchumi ulioigubika Afghanistan na hali mbaya ya maisha waliyonayo watu wa nchi hiyo, nchi za Magharibi zinazojinasibu kuwa zinajali haki za binadamu zimeamua kukata au kupunguza kila aina ya misaada ya kibinadamu kwa ajili ya Afghanistan kwa kisingizio kwamba itaupa nguvu na kuuimarisha utawala wa Taliban; msimamo ambao kwa mtazamao wa fikra za awaliowengi ndani na nje ya Afghanistan, haukubaliki.

Mbali na Iran kuipatia Afghanistan misaada ya kibinadamu, inafanya jitihada pia za kusaidia kurejesha uthabiti wa kisiasa nchini humo kwa kuishawishi serikali ya Taliban iunde serikali pana na jumuishi itakayosaidia kurejesha utulivu nchini humo.../

Tags