Jul 19, 2022 08:34 UTC
  • Tofauti kati ya safari ya Biden na Putin eneo la Asia Magharibi

Baada ya safari ya Rais Joe Biden wa Marekani katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu (Israel) na Saudi Arabia, Rais Vladimir Putin wa Russia leo yuko safarini nchini Iran. Kuna tofauti za wazi kati ya malengo na ajenda za safari ya Biden na Putin katika eneo la Asia Magharibi. Rais Tayyip Erdoğan wa Uturuki pia yuko safarani nchini Iran kwa lengo la mkutano wa pande tatu wa marais wa Iran, Russia na Uturuki.

Kuna tofauti kubwa kati ya ziara ya Biden katika eneo la Asia Magharibi na ziara ya Putin na Erdogan nchini Iran. Zaidi ya yote, Biden awali  aliingia katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na kisha Saudi Arabia kwa lengo la kukarabati  uhusiano na Saudi Arabia na kuishawishi nchi hiyo iongeze uzalishaji wake wa mafuta ya petroli. Aidha katika safari yake hiyo Biden alilenga kuishawishi Saudia iimarishe zaidi uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel na hali kadhalika kuunda muungano dhidi ya Iran. Kwa upande wa pili, Putin  amefika Tehran kwa ajili ya kuendeleza Mchakato wa Astana kuhusu  utatuzi wa mgogoro wa Syria na pia kwa ajili ya kuimarisha uhusiano na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Vikwazo vya Magharibi na hasa Marekani dhidi ya Iran na Russia pia ni nukta nyingine ambayo imepelekea nchi hizi mbili kuimarisha uhusiano ili kukabiliana na adui wa pamoja.

Suala jingine ni kwamba moja ya malengo ya Biden ya kusafiri katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu ambazo zimepachikwa jina la Israel na baada ya hapo kuelekea Saudi Arabia ni kuishinikiza zaidi Russia iafiki kushushwa bei ya mefuta ya petroli.

Kwa upande mwingine, moja ya malengo makuu ya ziara ya Rais Vladimir Putin mjini Tehran ni kuonyesha kwamba hayuko chini ya mashinikizo kutokana na vita vya Ukraine na kwamba sera za Marekani za kumtenga hazijafanya kazi, badala yake anaendelea kushindana na Marekani kieneo na kimataifa.

Hii ni mara ya pili kwa Vladimir Putin kuondoka Russia tangu kuanza kwa vita vya Ukraine. Chini ya mwezi mmoja uliopita, alisafiri hadi Ashgabat mji mkuu wa Turkmenistan kushiriki katika kikao cha kilele cha viongozi nchi za Pwani ya Bahari ya Kaspi na baada ya hapo akaenda Tajikistan.

Biden na Bin Salaman

Sasa, kuchaguliwa Tehran katika safari yake ya pili nje ya tangu kuanza kwa vita vya Ukraine kunatuma ishara hii kwa nchi za Magharibi kwamba sio tu kuwa Putin hajatengwa, bali anajaribu kuimarisha nafasi wake katika kambi ya Mashariki, na kwamba hatalegeza msimamo katika mashindano na madola mengine makubwa katika eneo la Asia Magharibi.

Kwa hakika, baada ya Biden kuzuru eneo na kutangaza kwamba Marekani haitajiondoa kutoka Asia Magharibi, alikuwa akijaribu kuzuia Russia na China kuimarisha zaidi ushawishi wao katika eneo hili. Katika safari yake mjini Tehran Putin atakuwa pia na mkutano wa pande mbili na Rais Recep Tayyip wa Uturuki na nukta hiyo inaashiria kuimarika uhusiano wa Moscow na nchi za eneo. Wakati wa safari yake mjini Tehran, Erdogan anatazamiwa kufanya mkutano wake wa kwanza wa ana kwa ana na rais wa Russia tangu kuanza kwa operesheni maalumu ya kijeshi ya Russia nchini Ukraine. Mkutano huo unaweza kupunguza hali ya  kudorora mahusiano kati ya Ankara na Moscow katika miezi ya hivi karibuni.

Suala jingine muhimu ni kwamba Biden alikuwa akifuata "mabadiliko" na "mgawanyiko" katika eneo la Asia Magharibi wakati wa safari yake. Njama hizo za Biden za kuibua fitina baina ya nchi za eneo zimekabiliwa na majibu hasi kutoka kwa nchi za eneo hili. Kwa maneno mengine ni kuwa mtazamo wa kihalisi wa nchi za eneo hili na hasa maelezo ya Faisal bin Farhan, Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudia aliposema kwamba "sijui NATO ya Waarabu ilitoka wapi", yanaonyesha kwamba mradi wa Marekani wa kueneza chuki dhidi ya Iran mara kwa mara umeshindwa. Umoja wa Falme za Kiarabu, Saudi Arabia, Misri na Iraq zimesema wazi kwamba hazitashiriki katika muungano wowote wa kijeshi dhidi ya Iran bali zinachotaka ni kuendeleza uhusiano mwema na Iran. Ni kwa msingi huo ndio hata wachambuzi wa Marekani wakaamini kuwa safari ya Biden katika eneo ilikuwa ni kosa kubwa na imefeli kufikia malengo yake. 

Katika safari yake Tehran, Putin hana lengo la kuingilia mambo ya nchi nyingine za eneo na wala hafuatilii muungano dhidi ya nchi yoyote, bali anataka kuimarisha uhusiano wa pande mbili na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Tags