Jul 26, 2022 04:42 UTC
  • Kuanza tena safari za Bin Salman katika nchi za Magharibi baada ya kusimama kwa miaka 4

Mohammed bin Salman, Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudi Arabia anatazamiwa kuondoka nchini humo leo Jumanne kwa ajili ya kufanya safari katika nchi za Ugiriki na Cyprus.

Imepita miaka 7 tangu Mohammed bin Salman aingie kwenye ngazi za juu za muundo wa mamlaka ya Saudi Arabia. Tangu 2015, Bin Salman amekuwa akihudumu kama Waziri wa Ulinzi wa Saudi Arabia na tangu 2017 kama Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa nchi hiyo. Kuanzia Juni 2017 hadi Oktoba 2018, Bin Salman alifanya juhudi kubwa kwa ajili ya kupata uhalali wa kufikia kiti cha ufalme wa Saudi Arabia kwa kusafiri katika nchi kadhaa za Magharibi na kujitambulisha kama mtu wa kwanza wa Saudi Arabia kimadaraka.

Hata hivyo, Bin Salman alifanya kosa kubwa Oktoba 2018. Mnamo Oktoba 2, 2018, Jamal Khashoggi, mwandishi habari wa Saudia aliyekuwa akifanyia kazi gazeti la Marekani la Washington Post, aliuawa kikatili katika ubalozi mdogo wa Saudia huko Istanbul, Uturuki, na mwili wake kukatwa vipande vipande. Katika saa za kwanza baada ya mauaji ya Khashoggi, vyombo vya habari vilitangaza kwamba uhalifu huo ulifanyika kwa amri ya Mohammed bin Salman. Radiamali ya serikali ya Uturuki, ambayo ilitangaza kwa njia isiyo ya moja kwa moja kwamba uhalifu huo ulifanyika kwa amri ya Muhammad bin Saman, iliongeza mashinikizo dhidi ya mwanamfalme huyo wa Saudia.

Bin Salman alituhumiwa pakubwa kuhusika na mauaji ya Khashoggi

Bin Salman, ambaye kabla ya jinai hiyo, alikuwa amefanya safari nyingi za nje, hususan katika nchi za Magharibi, baada ya jinai hiyo hakupata fursa ya kusafiri katika nchi yoyote ya Magharibi bali alisafiri katika baadhi ya nchi za Kiarabu tena kwa muda mfupi tu. Nchi pekee isiyo ya Kiarabu ambayo bin Salman aliitembelea katika kipindi hiki ilikuwa Uturuki, ambayo ilifanyika mwezi uliopita. Sasa, baada ya kupita miaka 4, mwanamfalme huyo wa Saudia amepangiwa kuzuru Ugiriki na kisha Cyprus siku ya Jumanne, ambayo ni safari yake ya kwanza katika nchi ya Magharibi baada ya kutokea mauaji ya Khashoggi.

Safari ya Ugiriki inaonyesha kuwa kwa sasa Bin Salman ametoka kwenye mashinikizo ya nchi za Magharibi. Mnamo tarehe 15 Julai, Rais Joe Biden wa Marekani alisafiri hadi Jeddah na kukutana na mwanamfalme huyo, ili kutoa ishara ya kumalizika mashinikizo ya nchi za Magharibi dhidi yake na pia kumruhusu aanze tena kufanya safari katika nchi hizo. Wakati wa kampeni zake za uchaguzi wa rais wa Marekani mwaka 2020, Joe Biden aliahidi kuifanya Saudi Arabia kuwa nchi iliyotengwa na kukataliwa kimataifa kufuatia mauaji ya Khashoggi, ahadi ambayo iliipuuza mwenyewe kivitendo kufuatia safari yake ya hivi karibuni huko Jeddah. Kwa sababu hiyo, wachambuzi wengi wanaamini kuwa Mohammed bin Salman ndiye amekuwa mshindi mkuu wa safari ya hivi karibuni ya Joe Biden katika eneo la Asia Magharibi.

Nukta nyingine ni kuwa safari ya Ugiriki na Cyprus ya Bin Salman inafanyika ili kuimarisha uhusiano wa Saudi Arabia na nchi hizo. Mwezi Oktoba mwaka jana, Mohammed bin Salman alimkaribisha Waziri Mkuu wa Ugiriki Kyriakas Mitsotakis mjini Riyadh. "Mkutano wa Pamoja wa Biashara wa Ugiriki na Saudi Arabia" pia ulifanyika Athens Mei mwaka jana. Wakati wa ziara ya mwanamfalme wa Saudia nchini Ugiriki, mikataba na makubaliano kadhaa katika nyanja za nishati, ushirikiano wa kijeshi na mawasiliano ya simu yatatiwa saini kati ya pande hizo mbili.

Biden katika safari yake ya karibuni Saudi Arabia

Suala jingine ni kwamba safari ya Ugiriki na kisha Cyprus ya Bin Salman inaweza kuwa ni mwanzo wa kufanyika safari nyingine kama hizo katika nchi nyingine za Magharibi ambapo zinaweza kutumika kama chombo cha kunufaika na siasa za kigeni kwa ajili ya kuimarisha nafasi yake katika muundo wa madaraka wa Saudi Arabia. Mwezi uliopita, Bin Salman pia alizitembelea nchi tatu za Misri, Jordan na Uturuki.

Tags