Jul 30, 2022 03:46 UTC
  • Macron akosolewa kwa 'kumtandikia zulia jekundu muuaji wa Khashoggi'

Wanaharakati na watetezi wa haki za binadamu wamemkosoa vikali Rais Emmanuel Macron wa Ufarasa kwa kumpokea Mrithi wa Ufalme wa Saudi Arabia, Mohammed bin Salman, ambaye anatuhumiwa kutoa amri ya kuuawa mwanahabari Jamal Khashoggi, huko nchini Uturuki miaka 4 iliyopita.

Agnès Callamard, Katibu Mkuu wa shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International amesema hatua ya mtawala huyo wa Saudia kuitembelea Ufaransa na vile vile Rais Joe Biden wa Marekani kuitembelea nchi hiyo ya Kiarabu haibadilishi ukweli kwamba, mwanamfalme huyo ni katili.

Callamard amemtaja mwanamfalme huyo wa Saudia mwenye umri wa miaka 36 kama mtu asiyewavumilia wapinzani na wakosoaji wa utawala wa kifalme wa Riyadh; na kwamba kurejeshwa kwake katika uga wa kimataifani undumakuwili na kukanyaga thamani za utu, kwa sababu tu ya hofu ya kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la kimataifa.

Wakati huohuo, Bénédicte Jeannerod, Mkuu wa shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch nchini Ufaransa, katika ujumbe wake wa Twitter amelaani kitendo cha Macron kuwa mwenyeji wa Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudia na kueleza kuwa, Macron anamsafisha na kuandaa mazingira ya kumrejesha Bin Salman katika jamii ya kimataifa, licha ya kuhusika na mauaji ya kinyama ya Jamal Khashoggi, kukandamizwa wakosoaji wa utawala wa Riyadh na jinai za kivita nchini Yemen. 

Macron akimpokea Bin Salman

Haya yanajiri siku chache baada ya Rais Joe Biden wa Marekani kusafiri hadi Jeddah na kukutana na mwanamfalme huyo, katika hali ambayo wakati wa kampeni zake za uchaguzi wa rais mwaka 2020, aliahidi kuifanya Saudia kuwa nchi iliyotengwa na kukataliwa kimataifa kufuatia mauaji hayo ya kikatili ya Khashoggi.

Mnamo Oktoba 2, 2018, Jamal Khashoggi, mwandishi habari wa Saudia aliyekuwa akifanyia kazi gazeti la Marekani la Washington Post, aliuawa kikatili katika ubalozi mdogo wa Saudia huko Istanbul, Uturuki, na mwili wake kukatwa vipande vipande. 

 

Tags