Aug 06, 2022 03:19 UTC
  • Jihad Islami yavurumisha makombora Israel baada ya kamanda wake kuuawa

Harakati ya Jihad Islami ya Palestina imevurumisha makombora zaidi ya 100 katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu zilizopachikwa jina la Israel ikiwa ni katika kulipiza kisasi hatua ya utawala katili wa Israel ya kumuua kamanda wa ngazi za juu wa harakati hiyo.

Jihad Islami imesema makombora hayo yaliyovurumishwa usiku wa kuamkia leo ni hatua ya awali tu ya kulipizia kisasi hujuma ya Israel ambayo imepelekea kuuawa watu 15 akiwemo kamanda huyo na mtoto wa miaka mitano mjini Rafah kusini mwa eneo la Ukanda wa Gaza ambalo liko chini ya mzingiro wa Israel.

Brigedi ya Quds tawi la kijeshi la Jihad Islami imetoa taarifa na kusema: "Kama hatua ya awali ya kuuawa kamanda mwandamizi Taysir al Jabari akiwa na mashahidi wenzake, Brigedi ya Al Quds imevurumisha makombora zaidi ya 100 jijini Tel Aviv, miji ya kati na miji iliyokaribu na Gaza."

Wizara ya Afya ya Palestina imesema zaidi ya watu 80 wamejeruhiwa katika hujuma hiyo ya Israel.

Katibu Mkuu wa Jihad Islami, Ziyad al-Nakhala amesema adui Muisraeli anapaswa kutarajia mapambano yasiyo na kikomo baada ya jinai ya Ijumaa.

Mpalestina aliyejeruhiwa katika hujuma ya Israel Ukanda wa Gaza

Amesema hakutakuwa na usitishaji vita kufuatia uchokozi huo wa Israel huku akisisitiza kuwa makundi yote ya kupigania ukombozi wa Palestina yanapaswa kupambana chini ya bendera moja.

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) ambayo pia iko na makao yake makuu Gaza imesema adui Muisraeli ametenda jinai mpya na lazima awajibishwe.

Mwezi Mei makundi ya muqawama ya kupigania ukombozi wa Palestina yaliyo Gaza yalivirumisha maroketi zaidi ya 4,000 kuelekea  Israel wakati wa Oparasheni ya Upanga wa al Quds baada ya utawala dhalimu wa Israel kuanzisha vita dhidi ya eneo hilo.

Jana Ijumaa Wapalestina waliandamana katika mji wa Ramallah katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel kulaani hujuma za utawala huo dhidi ya Gaza.