Aug 06, 2022 06:44 UTC
  • Iran yalaani hujuma ya Gaza iliyotekelezwa na utawala wa apathaidi wa Israel

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani hujuma ya kuogofya ya utawala wa apathaidi wa Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza na kusema: "Palestina ina haki ya kisheria ya kujilinda mbele ya hatua za kigaidi za Israel"

Ijumaa alasiri ndege za kivita za utawala haramu wa Israel zilishambulia Ukanda wa Ghaza na  kuua watu 15 akiwemo kamanda mwandamizi wa Harakati ya Jihad Islami,Taysir al Jabari, na mtoto wa miaka mitano mjini Rafah kusini mwa eneo hilo ambalo liko chini ya mzingiro wa Israel.

Katika taarifa, Nasser Kan'ani, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema hujuma ya utawala ghasibu wa Kizayuni ni jinai, uchokozi na uchochezi na kuongeza kuwa, utawala wa wa apathaidi wa Israel unabeba dhima ya matokeo mabaya ya uvamizi huo dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Ghaza.

Ameongeza kuwa, makundi ya mapamabano ya Palestina yana haki ya kisheria ya kujibu uvamizi na hatua za kigaidi za utawala wa Israel.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran aidha ametoa wito kwa nchi zote na taasisi za kimataifa kutekeleza majukumu yao ya kisheria na kimaadili katika kulinda taifa linalodhulumiwa la Palestina sambamba na kuzuia hatua za kigaidi za utawala wa Kizayuni ambao jinai zake ndio chanzo kikuu cha ukosefu wa uthabiti na usalama katika eneo la Asia Magharibi.

Katibu Mkuu wa Jihad Islami, Ziyad al-Nakhala

Kufuatia jinai hiyo, Harakati ya Jihad Islami ya Palestina imevurumisha makombora zaidi ya 100 katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu zilizopachikwa jina la Israel ikiwa ni katika kulipiza kisasi hatua ya utawala katili wa Israel ya kumuua kamanda wa ngazi za juu wa harakati hiyo.

Katibu Mkuu wa Jihad Islami, Ziyad al-Nakhala amesema adui Muisraeli anapaswa kutarajia mapambano yasiyo na kikomo baada ya jinai ya Ijumaa.

Tags