Aug 07, 2022 02:59 UTC
  • HAMAS: Kuanzisha uhusiano na Wazayuni ndio sababu ya kushadidi jinai dhidi ya Wapalestina

Msemaji wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema, mwenendo wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel ndio unaohamasisha utawala huo dhalimu kushadidisha jinai zake dhidi ya wananchi wa Palestina.

Hazim Qassem amefafanua kwa kusema: "utawala unaoikalia Quds kwa mabavu umeshadidisha jinai na dhulma zake dhidi ya wananchi na matukufu yetu tangu ulipoanzishwa mchakato wa kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala huo."

Hazim Qassem ameongeza kuwa, mapatano hayo ya kuanzisha uhusiano wa kawaida yanaushajiisha utawala wa Kizayuni kushadidisha jinai zake dhidi ya wananchi wa Palestina.

Kiongozi huyo mwandamizi wa Hamas amesisitiza pia kwamba utawala haramu wa Kizayuni wa Israel umekuwa, na utabaki kuwa adui namba moja wa taifa la Palestina na hiyo inaonyesha kuwa suala la Palestina litabaki kuwa kadhia kuu ya umma wote wa Kiislamu.

Hazim Qassem

Halikadhlika, msemaji wa harakati ya Hamas ameyataka mataifa ya Kiislamu yapaze sauti zao kupinga jinai za Wazayuni dhidi ya wananchi wa Palestina na kuungana pamoja kukabiliana na mradi wa Kizayuni unaolilenga taifa la Palestina na usalama wa taifa wa nchi za Kiarabu na Kiislamu.

Tangu siku ya Ijumaa iliyopita hadi sasa, utawala dhalimu wa Israel umefanya mashambulio ya anga mara kadhaa kulenga eneo la Ukanda wa Gaza, ambapo hadi sasa Wapalestina wasiopungua 13 wameshauawa shahidi na wengine 83 wamejeruhiwa.

Makundi ya Muqawama ya Palestina yametoa jibu kwa hujuma na mashambulio hayo ya kinyama ya Israel dhidi ya Gaza kwa kuvishambulia kwa makombora vitongoji vya walowezi wa Kizayuni vilivyoko kandokando ya Gaza na kusini mwa Tel Aviv.../

 

Tags