Aug 08, 2022 12:04 UTC
  • Raia Wapalestina 45 wameuawa shahidi katika siku 3 za hujuma za kikatili za Israeli huko Gaza

Siku tatu za mashambulizi ya utawala haramu wa Israel huko Gaza yamesababisha vifo vya raia Wapalestina 45 wakiwemo watoto 15 na wanawake wanne huku wengine 360 wakijeruhiwa

Hayo yameripotiwa baada ya mapatano ya usitishaji vita kutangazwa kuanzia saa tano usiku jana Jumapili kwa saa za Gaza (20:30 GMT).

Tangu Ijumaa, utawala wa Kizayuni wa Israel umekuwa ukishambulia Gaza kwa mabomu na kusababisha hasara kubwa katika maeneo ya raia.

Jeshi la Israel linadai kuwa limekuwa likiwalenga wanachama wa Harakati ya Jihad Islami wakiwemo makamanda wakuu wa kundi hilo lakini kulingana na maafisa wa Palestina, karibu nusu ya watu 44 waliokufa shahidi katika hujuma hizo za Israel ni raia.

Upatanishi wa Jumapili ulisimamiwa na Misri, kwa usaidizi wa Umoja wa Mataifa na Qatar. Katibu Mkuu wa Jihad Islami, Ziad al-Nakhala, amesema moja ya makubaliano muhimu ni hakikisho la Misri kwamba itajitahidi kuhakikisha kuwa viongozi wawili wa harakati hiyo wanaoshikiliwa mateka na Israel wanaachiliwa.

Katibu Mkuu wa Jihad Islami, Ziad al-Nakhala

"Jihad Islami imeweka masharti yake. Tunamtaka adui kumwachilia ndugu yetu ambaye amekuwa kwenye mgomo wa kula, Khalil Awawda, na pia kumwachilia Sheikh Bassem Al-Saadi," Al-Nakhala amewaambia waandishi wa habari katika mji mkuu wa Iran, Tehran.

Kukamatwa kwa Al-Saadi katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu wiki iliyopita ilikuwa mojawapo ya vichochezi vya hivi karibuni vya kushadidi taharuki.

Vikosi vya Israel vilitekeleza shambulizi Ijumaa katika Ukanda wa Gaza kufuatia kukamatwa kwake ili kuzuia mashambulizi ya kulipiza kisasi.

Makamanda wa Jihad Islam, Taysir al-Jabari na Khaled Mansour, waliuawa shahidi katika mashambulizi ya Ijumaa na Jumamosi, mtawalia.

Vikosi vya Israel pia vimewakamata wanachama wengine 19 wa Jihad Islami katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amepongeza hatua ya usitishaji mapigano huko Gaza huku akituma salamu za rambirambi kwa familia za waliouawa.