Aug 09, 2022 07:31 UTC
  • Msemaji wa Jihad al Islami: Wazayuni hawakutarajia Wapalestina wanaweza kujihami kiasi kile

Msemaji wa Harakati ya Jihad al Islami ya Palestina amesema kuhusu vita vya siku tatu vya Ghaza kwamba utawala wa Kizayuni unaoikalia kwa mabavu Quds tukufu umeemewa na haukutarajia kuwa Wapalestina wangeweza kujihami kiasi chote kile.

Jioni ya siku ya Ijumaa ya tarehe 5 Agosti, ndege za utawala wa Kizayuni zilianzisha mashambulizi dhidi ya baadhi ya maeneo ya Ukanda wa Ghaza na vita hivyo vya siku tatu vimepelekea Wapalestina 45 kuuawa shahidi na wengine 360 kujeruhiwa wakiwemo wanawake na watoto wadogo.

Makundi ya muqawama ya Palestina yalijibu jinai hiyo kwa kuitwanga miji na vitongoji vya Kizayuni kwa mamia ya makombora. Tel Aviv, mji mkuu wa utawala wa Kizayuni pamoja na uwanja wa ndege wa Ben Gurion pia ulipigwa kwa makumi ya makombora ya wanamapambano wa Palestina. Wazayuni 60 wamejeruhiwa na kuwahishwa hospitalini baada ya maeneo yao kutwangwa kwa makombora ya wanamapambano wa Palestina.

Israel inafanya jinai kubwa dhidi ya watoto wa Palestina

 

Tariq Izzuddin, msemaji wa harakati ya Jihad al Islami ya Palestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan alisema jana wakati alipohojiwa na shirika la habari la FARS kwamba, utawala wa Kizayuni ulidai kuwa umevunja nguvu za Brigedi za Quds, tawi la kijeshi la Jihad al Islami, lakini ulitahayari na kuemewa baada ya kukumbwa na majibu makali ya makombora kutoka kwa wanamapambano wa Palestina.

Amesema, utawala wa Kizayuni unatambua vyema kuwa, harakati ya Jihad al Islami ni kiungo muhimu sana cha muqawama wa Palestina huko Ghaza, Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Quds na kwamba medani zote hizo za mapambano haziwezi kutenganishwa wala kushindwa.