Aug 09, 2022 09:07 UTC
  • Nukta nne muhimu za hotuba ya Ashura ya Katibu Mkuu wa Ansarullah ya Yemen

Katibu Mkuu wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen amehutubia kwa mnasaba wa maadhimino ya Siku ya Ashura, hotuba ambayo ina ndani yake nukta nne muhimu za kutafakariwa.

Nukta ya kwanza katika hotuba ya Sayyid Abdulmalik Badruddin al-Houthi ni kwamba, adui amedhamiria kupotosha fikra sahihi za mafundisho ya dini. Upotoshaji ni tishio ambalo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei alishawahi kulizungumzia mara kadhaa hapo kabla. Upotoshaji ni kupindua na kugeuza ukweli na hakika ya mambo. Upotoshaji ni kufifisha mafanikio na kuzikuza kasoro na mapungufu. Upotoshaji umo katika uendelezaji wa vita vya kinafsi na kisaikolojia vya adui. Tishio hili linafanyiwa kazi katika nyuga kadhaa ikiwemo ya dini. Maadui wanaelewa vyema kwamba, dini ni kitendakazi cha kujengea umoja kwa jamii ya Kiislamu na ndiyo inayoipa utambulisho jamii hiyo. Kwa sababu hiyo, wanatumia kila mbinu, hasa kupitia mitandao ya kijamii ili kupotosha misingi ya dini na kufuatilia malengo yao yaliyo dhidi ya jamii ya Kiislamu hususan ya kuihodhi na kuiburuza. Kuhusiana na nukta hiyo, Katibu Mkuu wa Ansarullah amesema: "maadui wa umma wamedhamiria kupotosha fikra sahihi za mafundisho ya dini yetu ili kwa kuwapotosha Waislamu, wawakengeushe katika njia yao na kuwadhibiti."

 

Nukta ya pili katika hotuba ya Ashura ya Abdulmalik al-Houthi ni kwamba moja ya mafunzo muhimu zaidi ya Ashura kwetu sisi ni muqawama na kupambana kukabiliana na dhulma na uonevu. Muqawama ni fikra iliyopata nguvu zaidi hasa baada ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, lakini chimbuko na asili yake inarejea kwenye mapambano ya Ashura ya Imam Hussein (AS). Mapambano ndio stratejia muhimu zaidi iliyoinua nafasi ya mhimili wa muqawama katika eneo. Muqawama, kama tulivyoashiria, umepata ilhamu katika mapambano ya Ashura. Katika tukio la Karbala, Imamu huyo wa tatu wa Waislamu wa madhehebu ya Shia, hakukubali kuburuzwa na madhalimu, akakhitari na kuchagua njia ya muqawama na hatimaye akauawa shahidi kidhulma na kishujaa. Katibu Mkuu wa Ansarullah ameashiria funzo na somo hilo la Ashura kwa kusema: "hali halisi ilivyo inatufanya tufuate msimamo wa Imam Hussein (AS) wa kukabiliana na dhulma na uonevu na tusikubali katu kupigishwa magoti na kunyongeshwa."

 

Nukta ya tatu katika hotuba ya Ashura ya Sayyid Abdulmalik Badruddin al-Houthi ni kuhusu hatua ya baadhi ya nchi za Kiarabu ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni. Uanzishaji uhusiano huo umekuwa ukiendelea hadi sasa kwa sura rasmi na isiyo rasmi. Uanzishaji uhusiano rasmi na wa hadharani na utawala wa Kizayuni ni ule ulioanzishwa hasa na nchi mbili za Imarati na Bahrain Septemba 2020. Na uhusiano usio rasmi ni ule unaoendelezwa na Saudi Arabia, ambao ndio alioutilia mkazo zaidi Katibu Mkuu wa Ansarullah katika hotuba yake. Japokuwa Saudia haijatangaza hadharani kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na utawala haramu wa Israel, lakini umechukua hatua kadhaa zinazoonyesha kuwa inafuata mkondo huo kwa kasi kubwa. Kuhusiana na nukta hiyo Sayyid Abdulmalik al-Houthi amegusia hatua inazochukua Saudi Arabia kuhakikisha inakuwa na uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni na akasema: "Kuchaguliwa shekhe anayeunga mkono kufanya mapatano na Israel awe Khatibu wa Siku ya Arafa na kuwaruhusu Mayahudi waingie kwenye miji mitakatifu ya Makka na Madina ni kuyatusi na kuyavunjia heshima matukufu ya Kiislamu. Isitoshe, anga ya Saudi Arabia imefunguliwa kwa ajili ya Waisrael huku ikiwa imefungwa kwa wananchi wa Yemen."

Gil Tamari, mwandishi wa habari Myahudi aliyeruhusiwa kukanyaga ardhi ya Makka

 

Na nukta ya nne na ya kistratejia katika hotuba ya Al-Houthi ni kwamba, ghaya na lengo kuu la maadui ni kuhakikisha hatimaye wanaudhibiti na kuuburuza umma wa Kiislamu. Kuudhibiti na kuuhodhi umma wa Kiislamu ni suala ambalo maadui wa Magharibi na wa Kizayuni wamekuwa wakilifuatilia kwa miongo kadhaa na kwa mbinu tofauti. Hata hivyo kizuizi kikubwa kinachokwamisha njama yao hiyo ni nchi na mavuguvugu yanayopigania kuwa huru na kujivua na utegemezi na kuwa tayari kupambana na adui ili waweze kujitawala. Ni kwa sababu hiyo, maadui wa Uislamu, nao pia wanatumia kila njia kuziwekea mashinikizo nchi na makundi hayo ili yasiweze kujitawala na kujitegemea. Mojawapo ya malengo ya vita vya hizi majuzi vilivyoanzishwa na utawala haramu wa Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza ni hilo la kuuzuia muqawama wa Palestina usiweze kujitawala na kujitegemea. Sayyid Abdulmalik Badruddin al Houthi amekumbusha kwa kusema: "wakati maadui watakapoweza kuutenganisha umma wetu na uhuru na kujitawala halisi kunaoufanya usiwe na utegemezi kwao, hapo ndipo wataweza kuudhibiti umma wetu".../

Tags