Aug 10, 2022 07:44 UTC
  • Russia: Kuondoka majeshi ya Marekani Syria kutarahisisha na kuharakisha kuangamizwa magaidi

Mwakilishi wa kudumu wa Russia katika Umoja wa Mataifa amesema, kuondoka majeshi ya Marekani Syria kutarahisisha na kusahilisha kwa haraka zaidi kuangamizwa magaidi katika nchi hiyo.

Wanajeshi wa Marekani na magaidi wenye mfungamano nao, kwa muda sasa wamepiga kambi kinyume cha sheria ndani ya ardhi ya Syria, ambapo mbali na kupora maliasili ya mafuta na nafaka za nchi hiyo wanachukua hatua mbalimbali dhidi ya raia na vikosi vya jeshi la nchi hiyo.

Shirika la habari la TASS limeripoti kuwa Vassily Nebenzia ameyasema hayo alipohutubia kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kilichojadili tishio la ugaidi kwa amani na usalama wa kimataifa.

Nabenzia amesema, kuondoka majeshi vamizi ya Marekani katika ardhi ya Syria, kutakuwa na maana ya kuangamizwa haraka na kusikoweza kuepukika magaidi katika nchi hiyo na akaongezea kwa kusema, kutokomezwa maficho ya makundi ya kigaidi likiwemo la DAESH (ISIS) nchini Syria ni jambo la lazima.

Askari vamizi wa Marekani nchini Syria

 

Baada ya Marekani kuanzisha kile ilichokiita muungano wa kimataifa wa kupambana na Daesh, ililivamia na kulikalia kwa mabavu eneo la At Tanf, ambalo ni moja ya maeneo muhimu zaidi na ya kistratejia ya Syria na kuanzisha kituo cha kijeshi katika eneo hilo.

Viongozi wa Syria wameshasisitiza mara kadhaa kuwa hatua inazochukua Marekani ndani ya nchi hiyo ni sawa na "uvamizi na ukaliaji ardhi kwa mabavu".

Washington ndio muungaji mkono mkuu wa magaidi nchini Syria.

Mgogoro wa Syria ulianza mwaka 2011 kwa hujuma na mashambulio makali ya makundi ya kigaidi yaliyokuwa yakiungwa mkono na Saudi Arabia, Marekani na waitifaki wao kwa lengo la kubadilisha mlingano wa nguvu za kijeshi katika eneo kwa maslahi ya utawala haramu wa Kizayuni wa Israel. Mgogoro huo umesababisha Wasyria zaidi ya milioni 12 kuwa wakimbizi.

Pamoja na hayo, kwa msaada wa washauri wa kijeshi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na uungaji mkono wa Russia jeshi la Syria limeweza kulisambaratisha kundi la kigaidi la Daesh nchini humo.../

Tags