Aug 11, 2022 06:23 UTC
  • Je, ni nani mshindi hasa wa vita vya siku tatu huko Gaza?

Ikiwa ni katika kueneza siasa zake za kipropaganda, utawala wa Kizayuni wa Israel unaeneza uongo kuwa mara hii harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS haikushirikiana na harakati ya Jihad Islami katika vita vya siku tatu vya hivi karibuni huko Katika Ukanda wa Gaza.

Lakini ukweli wa mambo ni kwamba utawala huo unapuuza kwa makusudi nukta hii muhimu kuwa harakati ya Jihad Islamu peke yake imeweza kufikia uwezo wa kuuzuia utawala huo kuanzisha na kuendeleza hujuma dhidi ya Wapalestina, kwa kutilia maanani kuwa ikiwa huko nyuma uliweza kufikia makubaliano ya usitishaji vita na makundi kadhaa ya mapambano ya Kiislamu yakiongozwa na Hamas, lakini katika vita vya karibuni, harakati ya Jihad Islami imeweza kufikia hali hiyo ikiwa peke yake na kwa mtazamo huo, matokeo ya vita vya siku tatu, kinyume na unavyotangaza utawala wa Kizayuni, hayajakuwa na manufaa makubwa kwa utawala huo, na hasa ikizingatiwa kuwa harakati hiyo  imeweza kuulazimisha kumwachilia huru Khalil Awawdeh, mmoja wa viongozi wake wa ngazi za juu.

La muhimu zaidi ni kwamba katika vita hivyo sura halisi ya Yair Lapid Waziri Mkuu wa Utawala haramu wa Israel imedhihirika wazi zaidi mbele ya macho ya walimwengu.

Baadhi ya watoto waliouawa katika vita vya karibuni Gaza

Hapo awali, kwa sababu ya kutokuwa na rekodi ya kijeshi na kujihusisha na masuala ya vyombo vya habari na uandishi habari, wengi duniani walidhani kwamba Lapid angekuwa tofauti na watawala wengine wa mrengo wa kulia huko Israel, lakini sasa sura yake halisi ya kutenda jinai imedhihirika wazi katika vita vya karibuni. Baada ya kushuhudia unyama wake katika vita hivyo wengi wanakiri kwamba hana tofauti yoyote na watawala wengine wa mrengo wa kulia wa Israel kama vile Benjamini Netanyahu, bali hata huenda akawa ni mbaya zaidi kwani katika vita hivyo ambavyo vilijiri kwa maagizo yake, Wapalestina wasio na hatia wapatao 45, wakiwemo watoto 15 waliuawa na wengine 360 ​​wakajeruhiwa, huku zaidi ya makazi 1000 yakiharibiwa.

Kwa kutilia maanani kuwa kuna takriban watu milioni mbili na nusu wanaoishi katika Ukanda wa Gaza ulio na ukubwa wa kilomitamraba 350, na kutokana na ongezeko kubwa la watu, wengi wao ni watoto na vijana, hivyo ni vigumu bali ni jambo lisilowezekana kutenganisha baina ya ya maeneo ya wapiganaji wa kijeshi na raia wa kawaida katika ukanda huo. Hiyo ndiyo maana hatua yoyote ya kijeshi ya utawala wa Kizayuni katika eneo hilo daima huandamana na utendaji jinai za kivita.

Kwa mtazamo huo, ingawa Lapid huenda akajiona kuwa ni mshindi wa vita vya hivi karibuni kwa kuzingatia milinganyo ya kisiasa ya ndani ya Wazayuni,ambayo imepelekea umaarufu wake kuongezeka miongoni mwa Wazayuni wenye itikadi kali na walowezi wa ardhi za Wapalestina, lakini ukweli wa mambo ni kuwa nafasi yake imeharibika ulimwenguni, hasa machoni pa wale waliodhani kuwa angekuwa tofauti na watawala wengine wa mrengo wa kulia akiwemo Netanyahu. Kwa mtazamo huo vita vya siku tatu vya hivi karibuni huko Gaza vitaleta matokeo sawa kwa Lapid kama yale yaliyosababishwa na mashambulizi ya utawala wa Kizayuni kwenye kambi ya Qana huko kusini mwa Lebanon na ambayo yalitekelezwa kwa amri ya Shimon Peres.

Vile vile kuna uwezekano kwamba majeshi ya Kizayuni yalimburuza Lapid kwenye vita hivyo ili kuongezewa bajeti ya kijeshi, jambo ambalo ni sababu nyingine ya wazi inayothibitisha nafasi ya utawala huo katika kuanzisha vita hivyo. Kwa ujumla, kinyume na unavyodai na kueneza utawala wa Kizayuni, matokeo ya vita hivyo yamekuwa na madhara kwa utawala huo kwa mitazamo kadhaa. Kwa mtazamo wa kijeshi, harakati ya Jihad Islami peke yake imeweza kufikia mafanikio na uwezo mpya wa kuuzuia kuanzisha na kuendeleza hujuma dhidi ya Wapalestina na wakati huo huo kuulazimisha ukubali kusitisha mapigano.

Yair Lapid, Waziri Mkuu mtenda jinai wa Israel

Kimaadili, Lapid ameshindwa kabisa katika vita hivyo, ambapo sasa mikono yake imejaa damu ya raia na hasa watoto wa Palestina. Wengi wanaamini kuwa Lapid ni upande wa pili wa sarafu moja na Netanyahu. Kisiasa, vita hivyo na mauaji yaliyofuata yameziweka mahala pagumu nchi za Kiarabu zilizokuwa zikidai kwamba kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala huo kungepunguza makali ya jinai zake katika eneo. Bila shaka uungaji mkono wa moja kwa moja wa serikali ya Biden kwa utawala huo wa kigaidi pia umeharibu zaidi sura ya chama cha Democrat nchini Marekani.