Aug 12, 2022 12:33 UTC
  • Wanamichezo Wairaq wakataa kupambana na timu ya Israel katika mashindano ya Romania

Wanamichezo wawili Wairaqi wa mchezo wa tenisi wamekataa kupambana na wanamichezo kutoka utawala haramu wa Kizayuni wa Israel katika michuano ya Paralampiki inayofanyika nchini Romania.

Wanamichezo wengi wanaounga mkono Palestina katika nchi za Kiislamu na Kiarabu hawautambui utawala wa Kizayuni na hawako tayari kupambana na wapinzani wao wanaowakilisha Israel katika mashindano mbalimbali ya michezo.

Tovuti ya al-Ittijah imeripoti kuwa, Nasr Mahdi na Muhammad al-Mahdi, wachezaji wa mchezo wa Tenisi kutoka Iraq wamesusia kuchuana na wanamichezo wa utawala wa Kizayuni katika mashindano ya Paralampiki yanayofanyika nchini Romania.

Hii si mara ya kwanza kwa wanamichezo wa michezo mbalimbali kususia kupambana na wazayuni.

Mwanasoka wa timu ya taifa ya Algeria anasherehekea ushindi kwa bendera ya Palestina

 

Mapema mwezi huu wa Agosti, Badr al Hajri, bingwa wa mchezo wa sataranji kutoka Kuwait alighairi kushiriki mashindano ya kimataifa ya mchezo huo yaliyofanyika nchini Uhispania kwa kupangiwa kucheza na mpinzani kutoka Israel ili kuonyesha mshikamano na uungaji mkono kwa wananchi madhulumu wa Palestina.

Katika mashindano ya Olimpiki ya Tokyo, Japan pia baadhi ya wanamichezo walisusia kupambana na wanamichezo waliowakilisha utawala wa Kizayuni wa Israel. Katika mchezo wa Judo pekee, wanamichezo wawili kutoka Sudan na Algeria walijitoa kwenye mashindano hayo ili kuepuka kuchuana na wanamichezo kutoka Israel…/