Aug 13, 2022 01:30 UTC
  • Mapigano kati ya mamluki wa Saudia na UAE kusini mwa Yemen; kuendelea mzozo wa kijiografia na kisiasa

Wanamgambo wenye mfungamano na Umoja wa Falme za Kiarabu na Saudi Arabia wamepigana tena katika maeneo ya kusini mwa Yemen, hali ambayo imesababisha vifo na majeruhi kadhaa.

Tangu Machi 26, 2015, Yemen inakabiliwa na uchokozi wa muungano wa kijeshi wa Saudia. Saudia na Umoja wa Falme za Umoja wa Kiarabu UAE ndizo wanachama wakuu wa muungano huo. Baada ya muda, ilionekana wazi kuwa Saudi Arabia na UAE zingehitilafiana nchini Yemen na kushindana kupata ushawishi zaidi katika nchi hiyo. Kwa kuzingatia hilo, Riyadh na Abu Dhabi hivi karibuni zilikuwa na mzozo huko Yemen, ambapo muungano huo wa Saudi Arabia sasa umegawanyika na kuipelekea Saudia kujiendeshea mambo kivyake katika vita dhidi ya Yemen.

Kila moja ya nchi hizo ina vikosi vyake maalumu vinavyojitegemea nchini Yemen, ikiwa ni pamoja na vikosi vya kijeshi na makundi ya kisiasa. Vikosi vya serikali iliyojiuzulu ya Yemen vinaungwa mkono na Saudi Arabia na wanaotaka kujitenga katika Baraza la Mpito la Kusini nao wanaungwa mkono na UAE. Hadi sasa, kumekuwa na migogoro mingi kati ya mamluki wenye mafungamano na Saudi Arabia na UAE kusini mwa Yemen. Mapigano hayo yanathibitisha kwamba upande wa upinzani wa Serikali ya Kitaifa ya Wokovu ya Yemen yenye makao yake makuu huko Sana'a, mji mkuu, hauna umoja kama ilivyo hali  huko kaskazini na mji mkuu wa Yemen. Hali hiyo inaoonyesha wazi kuwa kuna wachezaji wengi katika eneo la kusini ambao wanafuatilia maslahi ya Saudi Arabia na UAE.

Majeshi ya UAE yakiwa katika ardhi ya Yemen

Mapigano ya karibuni yalitokea katika mkoa wa Shabwah. Huo ni mkoa wa pili kwa utajiri wa mafuta nchini Yemen baada ya Marib. Ukweli ni kwamba mkoa huo wa pwani na ambao una bandari ya mafuta umezifanya pande zinazozozana kusini mwa Yemen kuutazama mkoa huo na mafuta yake kwa jicho la tamaa. Adel al-Husseini, mmoja wa viongozi wa harakati ya mapambano ya kusini mwa Yemen, alisema hivi karibuni kufuatia jaribio la Imarati la kutaka kuudhibiti mkoa wa Shabwah kwamba: "Kwa vile Shabwah ni eneo lenye mafuta na utajiri mkubwa, Imarati na Saudi Arabia zinashindana kulidhibiti. Shabwah na sehemu nyingine kama hizo sio maeneo yenye migogoro. Hayo ni maeneo ya ushawishi, uwekezaji na mafuta."

Kwa hivyo, mizozo ya hivi karibuni inaonyesha kwamba ushindani kati ya Riyadh na Abu Dhabi na mamluki wao ungali unaendelea, na sasa nchi hizo na mamluki wao zinashindana kwa ajili ya manufaa na fursa za kiuchumi huko kusini mwa Yemen, na mashindano hayo yamesababisha migogoro mipya.

Suala jingine muhimu ni kwamba kuna mzozo kati ya mamluki wa Saudia na Imarati kusini mwa Yemen, huku usitishaji vita ukiwa umeanza kutekelezwa nchini tangu Aprili iliyopita. Wasaudi na Wayemen walifikia makubaliano ya usitishaji vita wa miezi miwili mwezi Aprili kwa upatanishi wa Umoja wa Mataifa, ambao ulirefushwa kwa mara ya tatu wiki iliyopita.

Manowari ya Saudia ikiwa katika pwani ya Yemen

Inaonekana kwamba usitishaji vita huo umepelekea tu kupunguzwa mashambulizi na migogoro ya kijeshi kati ya Saudia na Wayemeni, lakini wakati huo huo umeongeza ushindani wa kisiasa kati ya Saudi Arabia na Imarati kwa ajili ya kupata ushawishi zaidi kusini mwa Yemen. Kwa upande mwingine, mzozo kati ya mamluki wa Abu Dhabi na Riyadh kwa madhumuni ya kupata nguvu za kisiasa na kijeshi ungali unaendelea. Kwa hakika, usitishaji huo wa mapigano umechukuliwa na wavamizi wa Yemen na mamluki wao kuwa fursa nzuri ya kufuatilia maslahi yao ya kijiografia na kisiasa huko kusini mwa Yemen.

Tags