Aug 13, 2022 08:18 UTC
  • HAMAS yapongeza misimamo ya waziri wa ulinzi wa Pakistan dhidi ya Israel

Msemaji wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS amepongeza msimamo thabiti ulioonyeshwa na waziri wa ulinzi wa Pakistan dhidi ya utawala haramu wa Kizayuni wa Israel.

Waziri wa ulinzi wa Pakistan Khawaja Muhammad Asef ameieleza serikali ya Uingereza na waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo kuwa Azimio la Balfour la mwaka 1917 ndio chanzo cha machungu na mateso ya taifa la Palestina na kwamba mtu yeyote anayeunga mkono hatua za kigaidi za utawala wa Kizayuni ni mshirika wa utawala huo katika jinai unazowafanyia watu wa Palestina.

Katika taarifa iliyotolewa na msemaji wake Fawz Barhum Hamas imesema, misimamo ya waziri wa ulinzi wa Pakistan Khawaja Muhammad Asef inadhihirisha uungwana wa watu wa nchi hiyo na msimamo wao kuhusiana na kadhia ya Palestina ambayo ndiyo ajenda kuu ya umma wa Kiarabu na Kiislamu.

 

Taarifa hiyo ya Hamas imeongezea kwa kusema: "tunapongeza na kushukuru msimamo thabiti wa waziri wa ulinzi wa Pakistan na misimamo ya serikali na wananchi wa nchi hiyo katika kutetea piganio na lengo tukufu la Palestina".

Harakati ya Hamas imezitolea mwito pia nchi za Kiarabu na Kiislamu pamoja na mataifa mengine yanayotetea uhuru na ukombozi duniani kuchukua misimamo madhubuti dhidi ya utawala ghasibu unaoikalia Quds kwa mabavu pamoja na jinai unazotenda dhidi ya haki za wananchi wa Palestina, ardhi yao na matukufu yao ya Kiislamu na Kikristo.../

 

Tags