Aug 13, 2022 08:36 UTC
  • Sisitizo la Kiongozi Muadhamu kuhusu kuinuliwa hadhi ya Harakati ya Jihad Islami

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amejibu barua ya Katibu Mkuu wa Harakati ya Jihad Islami ya Palestina na kusema, "mapambano (muqawama) ya kishujaa ya Jihad Islami yatapelekea kupanda hadhi ya harakati hiyo katika mapambano sambamba na kusambaratisha hadaa za utawala wa Kizayuni na kuufedhehesha utawala huo."

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika kujibu barua ya Ziad al-Nakhalah, Katibu Mkuu wa Harakati ya Jihad Islami ya Palestina amesisitiza kuwa, nara zote za makundi ya Palestina katika ardhi zote za Palestina zinapaswa kuhimiza kulinda mshikamano na kuongeza kuwa: "Adui ghasibu anaendelea kudhoofika na harakati za mapambano ya Palestina zinaendelea kupata nguvu na sisi tunaendelea kuwa pamoja na nyinyi."

Ziad al-Nakhalah, Katibu Mkuu wa Harakati ya Jihad Islami hivi karibuni katika barua kwa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria kushiriki kwa wingi na kishujaa Mujahidina wa Palestina, hasa Harakati ya Jihad Islami na tawi lake la kijeshi, Brigedi za Quds, kote Palestina na hasa Gaza na Ukingo wa Magharibi na kusema:"Kwa uwepo wa brigedi za mapambano ya Jihad haipiti hata siku moja katika Ukingo wa Magharibi bila kuwepo makabiliano na utawala wa Kizayuni."

Katibu Mkuu wa Jihad Islami ameashiria hali ya Gaza na kusema kusimama kidete eneo hilo mkabala wa utawala ghasibu wa Israel na huku akibainisha kuhusu mapigano ya siku tatu ya hivi karibuni amesema: "Mapigano hayo tuliayapa jina la 'Wahda al-Sahat'  (Mshikamano katika Medani) ikiwa ni njia ya kusisitiza umoja wa taifa letu katika kukabiliana na adui ambaye anatumia njama na nguvu zake zote kusambaratisha umoja huu."

Ziad al-Nakhalah amesisitiza kuwa, katika vita hivyo maeneo yote ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina (zilizopachikwa jina la Israel) yalikuwa katika upeo wa makombora ya Jihad Islami na kuongeza kuwa: "Mapigano hayo yalisambaratisha tathmini za utawala wa Kizayuni kiasi kwamba utawala huo ulilazimika kuomba usitishaji vita baada ya siku tatu tu na haukuwa na budi ila kukubali masharti ya muqawama."

Wapiganaji wa Jihad Islami

Ayatullah Khamenei ameashiria nukta hiyo na kusema, matukio ya hivi karibuni yameongeza fahari ya Harakati ya Jihad Islami na kuinua hadhi ya harakati hii miongoni mwa harakati zingine shupavu za mapambano ya taifa la Palestina. Kwa muqawama wenu wa kishujaa, mumesambaratisha sera za  hadaa za utawala wa Kizayuni na kuufedhehesha utawala huo.  Mumeweza kuthibitisha kuwa kila kitengo cha muqawama kinaweza peke yake kumsambaratisha adui. Kwa kuunganisha mapambano ya Gaza na Ukingo wa Magharibi na vikosi vingine vya muqawama na uungaji mkono wao kwa harakati ya Jihad Islami, mumeweza kuonyesha mshikamano wa jihadi ya taifa la Palestina mbele ya adui muovu na mdanganyifu. Jitihada  zote za makundi ya Palestina katika ardhi zote za Palestina zinapaswa kujikita katika kuhimiza kulinda mashikamano. Adui ghasibu anaendelea kudhoofika na harakati za mapambano ya Palestina zinaendelea kupata nguvu.

Ushauri wa Ayatullah Khamenei kuhusu ulazima wa kuwepo umoja na mashikamano wa makundi yote ya Palestina una umuhimu hasa kwa kuzingatia kuwepo njama za utawala wa Kizayuni za kuibua mifarakano baina ya makundi ya Jihadi ya Palestina. Katika mwanzo wa vita dhidi ya Gaza Ijumaa iliyopita, utawala wa Kizayuni ulisema lengo la vita hivyo lilikuwa ni kukabiliana na harakati ya Jihad Islami pekee. Pamoja na hayo, ushujaa wa Jihad Islami katika mapambano ni jambo ambalo limeyashangaza makundi mengine ya muqawama au mapambano katika eneo na dunia nzima na katika taifa la Palestina, makundi yote ya muqawama yakiongozwa na Hamas yameunga mkono Jihad Islami. Kwa hivyo, kinyume na walivyotaka watawala wa Tel Aviv, makundi yote  ya Palestina yameunga mkono Jihad Islami.

Nembo za Hamas na Jihad Islami

Nukta nyingine muhimu katika barua ya Katibu Mkuu wa Jihad Islami ni shukrani zake kwa Iran kutokana na uungaji mkono wake kwa makundi yanayopigana Jihadi huko Palestina. Katibu Mkuu wa Jihad Islami ameyataja mafanikio hayo ya muqawama kuwa ni utangulizi wa ushindi mkubwa zaidi kwa taifa la Palestina katika siku zijazo na akashukuru nafasi ya harakati ya Hizbullah chini ya uongozi wa Seyed Hassan Nasrallah, pamoja na uungaji mkono na ridhaa ya Iran katika nyanja zote chini ya uongozi na muongozo wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu. Katibu Mkuu wa Jihad Islami ya Palestina amesema bila ya uungaji mkono na kusimama  kidete bila kikomo Iran na Hizbullah, ushindi huu na ushindi mwingine uliopita haungepatikana.

Kwa muda mrefu sasa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikiunga mkono kwa pande zote malengo ya taifa la Palestina katika kukabiliana na utawala wa Kizayuni na uungaji mkono huo ni msingi muhimu katika sera zake za kigeni.

 

Tags