Aug 14, 2022 02:31 UTC
  • Magaidi 50 wa Daesh wahamishiwa Iraq kutoka nchini Syria

Kitengo cha upashaji habari cha jeshi la Iraq kimetoa ripoti rasmi na kusema kuwa karibu wanachama 50 wa genge la kigaidi na ukufurishaji la Dashe (ISIS) wamehamishiwa mkoani Nainawa (Nineveh) Iraq kutoka katika kambi ya al Hawl ya nchini Syria.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, hivi sasa kuna takriban wakazi 56,000 katika kambi ya al Hawl huko Syria. Kambi hiyo ni maarufu kwa jina la bomu la saa kwani sehemu kubwa ya magaidi ISIS bado wako kwenye kambi hiyo hasa familia za magaidi hao. Iko kaskazini mashariki mwa Syria katika umbali wa kilomita 10 kutoka mpaka wa Iraq.

Kamati ya upashaji habari ya jeshi la Iraq imesema pia katika tamko lake hilo rasmi kwamba, jeshi hilo limepokea magaidi wapatao 50 wenye uraia wa Iraq baada ya kutiwa mbaroni nchini Syria. Tamko hilo limeongeza kuwa, serikali ya Syria imewakabidhi magaidi hao kwa jeshi la Iraq kupitia mpaka wa Rabia ili shirika la kijasusi na upelelezi la serikali ya shirikisho la Iraq linalofanya kazi chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi hiyo lifanye upelelezi wake kuhusu magaidi hao ili baadaye wachukuliwe hatua zinazotakiwa.

Kambi ya al Hawl ya nchini Syria ambayo sehemu yake kubwa ina familia za magaidi wa ISIS

 

Juzi Ijumaa usiku pia, familia 150 za magaidi wa ISIS ambazo zina watu 620 zilikabidhiwa kwa kambi ya al Jeddah ya Iraq. Duru za kiusalama zinasema kuwa, wengi wa watu wa familia hizo za magaidi wa Daesh waliohamishiwa kwenye kambi hiyo ya al Jeddah ya Iraq ni wanawake na watoto.

Wakuu na wakazi wa mkoa wa Nianawa huko Iraq wanapinga sana kurejeshwa Wairaq hao kwenye mkoa wao kutokana na kuwa ni familia za magaidi wa ISIS waliofanya jinai kubwa ndani na nje ya nchi za Syria na Iraq, lakini serikali ya Iraq inasema haina chaguo jengine isipokuwa kuwapokea na kuwaweka kambini.

Tags