Aug 14, 2022 11:21 UTC
  • Marekani yashadidisha vitendo vyake vya ujasusi nchini Iraq

Ndege za Marekani hivi sasa zimeanzisha operesheni nyingi za kijasusi ambazo hazijawahi kushuhudiwa tangu walipoivamia na kuikalia kwa mabavu Iraq mwaka 2003. Operesheni hizo zimejikita katika kambi ya kijeshi ya Ain al Assad kuelekea ndani ya ardhi ya nchi jirani ya Syria.

Taarifa zinasema kuwa, katika kipindi cha miezi ya hivi karibuni, kambi za kijeshi za Marekani katika maeneo ya mpakani mwa Syria na Iraq zinashuhudia harakati za kijasusi ambazo hazijawahi kutokea. Kambi hizo huwa zinashambuliwa mara kwa mara kwa makombora.

Shirika la habari la al Maaluma la Iraq limemnukuu afisa mmoja wa masuala ya usalama wa mkoa wa al Anbar wa magharibi mwa Iraq akifichua habari hiyo leo Jumapili na kuongeza kuwa, askari wa Marekani wameanzisha operesheni kubwa sana ya kijasusi na operesheni hiyo imejikita katika kambi ya jeshi la anga ya Ain al Assad katika eneo la al Baghdadiyyah la magharibi mwa mkoa wa al Anbar.

Maandamano ya kupinga jinai, ujasusi na ubeberu wa Marekani nchini Iraq

 

Afisa usalama huyo wa Iraq ameongeza kuwa ndege kadhaa za kivita za Marekani zimetua kwenye kambi hiyo ingawa hata hivyo haikutangazwa lengo la hatua hiyo na ni kitu gani hasa muhimu kimepelekwa ndani ya kambi ya Ain al Assad kwa kutumia ndege hizo za kivita za Marekani.

Kabla ya hapo pia jeshi la Marekani lilikuwa tayari limeshadidisha na kuweka ulinzi mkali kwenye kambi ya jeshi la anga ya Ain al Assad kiasi kwamba limepiga marufuku gari yoyote ya kijeshi kukaribia kambi hiyo na haisiti kuishambulia gari yoyote ya deraya inayokaidi amri ya kutoikaribia  kambi hiyo.