Aug 15, 2022 10:17 UTC
  • Balozi mpya wa Kuwait aaanza kufanya kazi nchini Iran baada ya miaka 7

Badr Abdullah Al-Manikh, balozi mpya wa Kuwait katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Jumamosi, mwanzoni mwa kazi yake, alikutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Hossein Amir Abdullahian, na kumkabidhi nakala ya vitambulisho vyake.

Katika miezi ya hivi karibuni, baadhi ya nchi za Kiarabu za eneo la Ghuba ya Uajemi, zikiwemo Kuwait na Umoja wa Falme za Kiarabu, ambazo zina hamu ya kudumisha uhusiano wa ujirani mwema na Iran, zimetangaza nia yao ya kuboresha uhusiano na serikali ya Iran. Saudi Arabia nayo pia imebainisha kuridhika na mchakato wa sasa wa mazungumzo na Iran chuni ya upatanishi wa Iraq.

Mnamo 2016, baada ya matukio yanayohusiana na ubalozi wa Saudia mjini Tehran na ubalozi mdogo wa nchi hiyo mjini Mashhad kaskazini mashariki mwa Iran, Kuwait, sawa na baadhi ya nchi za Kiarabu, katika kupinga tukio hilo na kuunga mkono Saudi Arabia, ilipunguza kiwango cha Mahusiano ya kisiasa na Tehran. Sasa, baada ya miaka 7, Kuwait imeamua kurejesha mahusiano na Iran katika ngazi ya balozi.

Uhusiano na maingiliano ya Kuwait na Iran katika miaka ya hivi karibuni, licha ya masuala na changamoto mbalimbali za kieneo, yamekuwa na mwelekeo thabiti na endelevu. Katika migogoro ya kikanda, Kuwait na Iran zimepunguza kiwango cha uhusiano wao, lakini hazijawahi kukata uhusiano wao.

Katika miaka ya hivi karibuni, Kuwait imejaribu kudumisha uhusiano wenye uwiano na Iran na Saudi Arabia ili kulinda maslahi yake. Kuwait ikiwa ni moja ya nchi zenye watu wachache ambazo nyingi zinaundwa na wahamiaji; Ni jirani na madola matatu yenye ushawishi ya Iran, Saudi Arabia na Iraq, ambayo yameibua fursa na vitisho kwa nchi hiyo, na kwa hiyo, serikali ya Kuwait daima imekuwa ikitilia mkazo ulazima wa kuwepo uhusiano wa amani unaozingatia ujirani mwema na nchi za eneo.

Sheikh Ahmed Nasser Al-Sabah, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Kuwait tarehe 26 Julai katika mazungumzo ya simu na Hossein Amir- Abdullahian sambamba na kushukuru mpango wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kuendeleza uhusiano na nchi za eneo hili, alisisitiza juu ya suala la kupanua zaidi uhusiano wa pande mbili kati ya Kuwait na Tehran. Aliendelea kusema:  Uongozi wa kisiasa wa Kuwait siku zote umekuwa ukitaka kuimarisha uhusiano na Iran, na uteuzi wa balozi mpya wa Kuwait nchini Iran uko katika mwelekeo huu."

Sheikh Ahmed Nasser Al-Sabah, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Kuwait

Kwa hakika, tofauti katika mahusiano ya Iran na Kuwait, ambazo huathiriwa zaidi na pande tatu, inaweza kuchukuliwa zaidi kuwa ya mpito; Kwa mfano, mara tu baada ya kumalizika vita vya kulazimishwa vya Iraq dhidi ya Iran mwaka 1988, Kuwait ilifungua ubalozi wake mjini Tehran, na mwaka 1390, Iran ilikuwa nchi ya kwanza kulaani hatua ya Iraq  kuivamia na kuikalia kwa mabavu Kuwait. Iran ilimtaka mtawala wa wakati huo wa Iraq, Saddam, aondoe jeshi lake vamizi nchini Kuwait.

Serikali ya Kuwait pia imejaribu kuchukua nafasi katika kutafuta suluhu za kisiasa kutatua migogoro ya kikanda katika miaka ya hivi karibuni; Nchi hii pia inapinga uhalalishaji wa uhusiano wowote na utawala wa Kizayuni, na baada ya kuanzishwa uhusiano wa kawaida  kati ya Imarati na utawala wa Kizayuni, mashirika mengi yasiyo ya kiserikali na bunge la Kuwait walilaani kitendo hicho.

Ni dhahiri kuwa baada ya Marekani na utawala wa Kizayuni kushindwa kujenga muungano dhidi ya Iran katika eneo, sasa inaonekana nchi za Kiarabu zinachukua hatua za kuendeleza uhusiano wao na Iran; Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa ikitilia mkazo ulazima wa maelewano kuwa ni sharti la usalama na uthabiti na vile vile mdhamini wa maslahi ya mataifa ya eneo hili.

Kwa kuzingatia hayo, kuchaguliwa balozi mpya wa Kuwait nchini Iran na kutilia mkazo viongozi wa nchi hizo mbili juu ya ulazima wa kuimarishwa uhusiano kunaweza kutathminiwa kuwa ni ahadi ya sura mpya ya uhusiano kati ya nchi hizo mbili.

Siasa za kigeni za serikali ya 13 ya Iran zinalenga katika kuboresha uhusiano na nchi jirani na za Kiislamu za eneo la Ghuba ya Uajemi; Mbali na kuzidisha uhusiano wa kiuchumi na kiusalama wa Tehran na nchi za eneo, jambo hili linaweza kusaidia kuutenga utawala wa Kizayuni na kushindwa njama za utawala huu na Marekani za kuitenga Iran.

Seyed Ebrahim Raisi, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran tarehe 4 Mei katika mazungumzo ya simu na Amir wa Kuwait, Al-Ahmad Al-Jaber Al-Sabah, alielezea misimamo ya nchi hii kuhusiana na njama za kieneo, na kwa akikumbushia uhusiano mzuri kati ya Iran na Kuwait huko nyuma, amesisitiza kuwa: Uhusiano kati ya Iran na Kuwait ikiwa ni marafiki wawili wa zamani unapaswa kurejea katika uwezo wao wa kweli.