Aug 15, 2022 10:37 UTC
  • DAESH (ISIS) wametumia asilimia 90 ya silaha za Marekani katika operesheni za kigaidi

Mtaalamu mmoja wa masuala ya kiusalama amesema, asilimia 90 ya wahanga na waathirika wa ugaidi nchini Iraq hasa katika maeneo yaliyokombolewa wameuliwa kwa silaha za Marekani.

Japokuwa kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh limeshindwa na kusambaratishwa katika nchi za Iraq na Syria, mabaki ya magaidi wa kundi hilo yangaliko katika nchi hizo na Marekani ingali inatoa msaada na uungaji mkono kwa magaidi hao.

Tovuti ya habari ya al Maalumah imeripoti kuwa Shahin al Ubaidi, mtaalamu wa masuala ya kiusalama amesema, kuna ongezeko kiasilimia la kiwango cha silaha za Marekani zinazotumiwa na magaidi katika mashambulio wanayofanya dhidi ya raia au maeneo ya kijeshi, iwe ni katika mkoa wa Diyala au mikoa mingine ya Iraq.

 

Al Ubaidi ameongeza kuwa, asilimia 90 ya waathirika wa ugaidi nchini Iraq wameuliwa kwa silaha za Marekani hasa za utunguaji, ambapo kwa sasa idadi hiyo ni asilimia 60 ya wahanga wote.

Mtaalamu huyo wa Kiiraq wa masuala ya kiusalama amebainisha kuwa, kutumia Daesh silaha za Marekani na njia zilizotumika kufikishwa silaha na zana hizo za kivita kwenye maficho ya kundi hilo la kigaidi, yote hayo ni masuali ambayo majibu yake yanahitaji utafiti, kwa sababu yatafichua siri nyingi katika uga wa kiusalama wa Iraq.

Inafaa kuashiria hapa kuwa, mbunge wa Syria Muhammad Fawaz alisema jana kuwa, Marekani inawaruhusu magaidi wa DAESH (ISIS) kuongeza kiwango cha shughuli na harakati zao hadi karibu na mipaka ya Syria na Iraq na kwamba hivi sasa hakuna asiyejua kuwa Washington inalihami na kuliunga mkono kundi hilo la kigaidi.../

Tags