Aug 16, 2022 02:41 UTC
  • Karzai: Wananchi wa Afghanistan wametaabika mno kwa kuweko majeshi ya Marekani nchini kwao

Hamid Karzai Rais wa zamani wa Afghanistan amesema kuwa, wananchi wa nchi hiyo wamedhurika pakubwa katika kipindi cha miaka 20 iliyopita ya kuweko majeshi ya kigeni yakiwemo ya Marekani katika nchi yao.

Karzai amesema hayo katika mahojiano maalumu aliyofanyiwa na chombo kimoja cha habari cha India ambapo sambamba na kuzungumzia matukio ya mwaka mmoja uliopita nchini Afghanistan ameashiria madhara makubwa waliyoyapata wananchi wa nchi hiyo kutokana na kuweko majeshi ya kigeni katika ardhi ya nchi yao.

Karzai ambaye alioongoza Afghanistan akiwa Rais kuanzia mwaka 2002 hadi 2014 ameeleza kuwa, licha ya kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, vitendo vya utumiaji mabavu nchini Afghanistan vimepungua na watu hawafi sana, lakini katika miaka 20 iliyopita hususan mwaka jana, nchi hiyo imekabiliwa na matatizo ya kiuchumi na wenye vipawa kuhajiri na kuihama nchi hiyo.

Baadhi ya viongozi wa kundi la Taliban

 

Aidha amesema, ukiondoa suala la usalama, katika mwaka mmoja uliopita, Afghanistan imekabiliwa na matatizo chungu nzima na kwamba, njia pekee ya utatuzi wa hayo ni kuundwa serikali jumuishi na kuacha sheria ifuate mkondo wake.

Kuhusiana na suala la kutambuliwa rasmi serikali ya wanamgambo wa Taliban, Hamid Karzai amesema kuwa, ili Taliban ikubaliwe na jamii ya kimataifa, awali ya yote inapaswa kuheshimu sheria za raia ndani ya nchi kama vile kufungua shule za wasichana na kuunda serikali jumuishi hatua ambazo bila shaka zitaifanya serikali yake ikubaliwe na wananchi na kwa msingi huo itakuwa imepiga hatua kuelekea kutambuliwa kimataifa.