Aug 16, 2022 14:04 UTC
  • Israel yakiri kuwaua watoto  Wapalestina Gaza

Utawala wa Kizayuni wa Israel umekiri kuwaua watoto watano Wapalestina katika hujuma yake ya hivi karibuni dhidi ya Ukanda wa Gaza.

Utawala huo dhalimu ulianzisha  vita dhidi ya Gaza mnamo Agosti 5 na vita hivyo vilimalizika baada ya siku tatu kufuatia upatanishi wa Misri.

Jumla ya watu 49 waliuawa shahidi katika hujuma hiyo ya Israel dhidi ya Gaza katika kipindi hicho wakiwemo watoto 17 huku mamia ya wengine wakijeruhiwa.

Watoto watano waliuawa katika siku ya mwisho ya vita hivyo wakati ndege za kivita za Israel ziliposhambulia eneo la Jabalya.

Awali Israel ilidai kuwa watoto hao waliuawa kwa kombora la Harakati ya Jihad Islami bila kutoa ushahidi lakini sasa  utawala huo umelazimka kukiri ndio uliotekeleza jinai hiyo.  Watoto waliouawa shahidi katika shambulio hilo la kinyama la Israel wametajwa kuwa ni Jamil al-Din Nijm, 3; Jamil Ihab Nijm, 13; Mohammad Nijm, 16; Hamed Nijm, 16; na Nathmi Karsh, 15.

Watoto watano Wapalestina waliouawa katika hujuma ya Israel Gaza

Katika kujibu jinai ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Gaza, Harakati ya Jihad Islami ilivurumisha mamia ya makombora kuelekea ardhi zinazokaliwa kwa mabavu ambazo zimepachikwa jina la Israel na kuwasababishia Wazayuni hasara kubwa.

Utawala katili wa Israel umeanzisha vita mara tano dhidi ya Gaza tokea mwaka 2008 ambapo hutumia zilaha ilizopewa na Marekani kuwaua kwa umati raia wa Palestina.