Aug 17, 2022 02:34 UTC
  • Iraq katika mkondo wa kushtadi zaidi mkwamo wa kisiasa

Uamuzi wa makundi na mirengo ya kisiasa ya Iraq wa kufanya mikusanyiko ya barabarani umeifanya anga ya kisiasa ya nchi hiyo kuwa tete zaidi na mkwamo wa kisiasa unaoikabili nchi hiyo kushtadi zaidi.

Iraq imeendelea kushuhudia mkwamo wa kisiasa kwa miezi kumi sasa ambao chimbuko lake ni matokeo ya uchaguzi wa Bunge uliofanyika Oktoba mwaka jana 2021. Hakuna mrengo wowote au hata waitifaki wao waliofanikiwa kupata viti vya Buunge ambavyo vinawapa uwezo na mamlaka ya kisheria ya kuteua Rais na Waziri Mkuu. Mintarafu hiyo, katika mazingira kama haya hakukuwa na njia nyingine ya kuunda serikali isipokuwa kupitia njia ya mazungumzo kwa minajili ya kufikia mwafaka wa kisiasa. Hata hivyo mgawanyiko ulioibuka miongoni mwa mirengo ya kisiasa ya nchi hiyo kivitendo umekwamisha na kuwa kigingi katika njia ya mazungumzo. Hali hii imeifanya Iraq kuutumbukia katika mkwamo mrefu zaidi wa kisiasa tangu kuondolewa madarakani utawala wa dikteta Saddam.

Katika siku za hivi karibuni kumejitokeza masuala mawili nchini Iraq: Mosi, mwito wa kufanyika uchaguzi wa mapema wa Bunge na pili, mikusanyiko katika barabara mbalimbali za nchi hiyo. Kufanyika uchaguzi wa mapema wa Bunge na kuwaleta barabarani wafuasi ni mambo ambayo yameibuliwa na kutekelezwa na mrengo wa al-Sadr. Mrengo wa al-Sadr ambao ulijikusanyia viti 73 katika uchaguzi wa Bunge, ulitangaza kujiengua Bungeni baada ya kushindwa kuunda serikali kwa mujibu wa matakwa yake. Aidha Muqtada Sadr kiongozi wa harakati ya al-Sadr alitangaza kuiondoa harakati hiyo katika uga wa kisiasa nchini humo.

Bunge la Iraq

 

Inaonekana kuwa, kuibuliwa suala la kuitishwa uchaguzi wa mapema wa Bunge, ni juhudi za Harakati ya al-Sadr na kiongozi wake za kutaka kuweko tena katika medani ya siasa za Iraq. Uwepo huu wa mara nyingine lengo lake ni kutaka kujinyakulia viti zaidi vya Bunge kupitia uchaguzi wa mapema na kutekeleza lengo la hapo kabla ambalo ni kuunda serikali kwa mujibu wa utashi na matakwa yake.

Pendekezo la kufanyika uchaguzi wa kabla ya wakati limepokewa kwa mikono miwili na baadhi ya makundi na mirengo ya kisiasa ya Iraq huku baadhi ya mirengo na shakhsia kama Nourio al-Maliki aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wakipinga vikali hilo. Wanaopinga kufanyika uchaguzi wa kabla ya wakati wanasema kuwa, madhali misingi ya kisiasa na malengo ya kisiasa ya makundi na mirengo mingine nchini Iraq hayajakubaliwa na kuheshimiwa na wakati huo huo kungali kuna hali ya kuhodhi anga na ulingo wa siasa, hata kukifanyika uchaguzi mwingine, hilo haliwezi kuiondoa nchi hiyo katika mkwamo wa kisiasa ilionasa ndani yake na badala yake itakuwa ni kuzidi kulitwisha tu taifa hilo mzigo wa gharama.

Harakati ya al-Sadr ikiwa na lengo la kushinikiza takwa lake yaani la kufanyika uchaguzi wa mapema wa Bunge imekimbilia katika kuwahamasisha wafuasi wake wajitokeze na kufanya mikusanyiko barabarani na hivyo kutaka kuonyesha kwamba, ina himaya ya jamii.

Muqtada al-Sadr, Kiongozi wa Harakati ya al-Sadr ya Iraq

 

Ni katika mkondo huo, ndio maana Harakati ya al-Sadr imeitisha mkusanyiko mkubwa wa mamilioni ya watu Jumamosi ijayo. Mkabala na hatua hiyo, kumetolewa mwito wa kujitokeza mamilioni ya Waislamu wa madhehebu ya Shia kwa minajili ya kutetea utulivu na usalama  wa nchi na heshima ya asasi zenye mamlaka ya uongozi nchini Iraq.

Hapana shaka kuwa, mbinu hii sio tu kwamba, haitakuwa na msaada wowote katika kuikwamua nchi hiyo na mkwamo wa sasa wa kisiasa, bali inashadidisha mkwamo huo na wakati huo huo, maadui wa Iraq wakitumia nguvu ya vyombo vyao vya habari wanafanya njama za kuipaka matope mirengo ya Waislamu wa madhehebu ya Shia na kuichafua mbele ya fikra za waliowengi.

Ukweli wa mambo ni kuwa, kile ambacho kinahitajika kwa sasa nchini Iraq ni ukomavu na akili ya kisiasi ya mirengo na makundi ya nchi hiyo sambamba na kutanguliza mbele maslahi ya kitaifa badala ya maslahi ya kimirengo; na lengo hili kwa hakika haliwezi kufikiwa pasi na kuweko mazungumzo ya dhati ya kisiasa baina ya mirengo hiyo.

Tags