Aug 17, 2022 02:40 UTC
  • Wapalestina wafichua njama ya Israel ya kuubomoa kikamilifu msikiti wa Al Aqsa

Duru za Palestina katika mji wa Baitul Muqaddas (Jerusalem) unaokaliwa kwa mabavu zimefichua njama ya awamu tatu iliyoandaliwa na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel kwa lengo la kuubomoa msikiti mtukufu wa Al Aqsa.

Kwa mujibu wa duru hizo, lengo la njama hiyo ni kuchimba misingi kwa madhumuni ya kuzifanya kuta za msikiti wa Al Aqsa na ardhi ya kandokando yake zilegelege hatua kwa hatua mpaka hatimaye msikiti huo uporomoke kikamilifu.

Ripoti iliyotolewa na duru za Palestina imebainisha kuwa, njama hiyo ya utawala wa Kizayuni ni ya awamu tatu, ambapo awamu na hatua zake mbili za mwanzo zinajumuisha uchimbaji na uondoaji udongo ili kuzifanya kuta za msikiti wa Al Aqsa zilegelege na kuendelea kuchimba mashimo chini ya misingi ya msikiti huo kwa lengo la kuhakikisha hatimaye unaporomoka.

Mwendelezo wa uchimbaji mashimo na misingi hiyo ulioanza tangu miaka kadhaa nyuma umesababisha kulegalega kuta za msikiti wa Al Aqsa; mfano ambao umeshuhudiwa hapo kabla katika ukuta wa upande wa kusini wa msikiti huo kwa katika urefu wa mita 30.

 

Kwa mujibu wa ripoti ya duru za Palestina, hatua ya tatu ya njama hiyo ni kuzuia kuta za msikiti wa Al Aqsa zisifanyiwe matengenezo na ukarabati kwa namna itakayopelekea kila baada ya muda kuporomoka mawe ya msikiti huo na ya kuta za kandokando yake.

Uporomokaji huo umeanza kutokea hasa katika eneo la kusini na kusini magharibi ya msikiti wa Al Aqsa; na sababu kuu ni hatua za Wazayuni maghasibu za kuhakikisha wanapenya ndani ya msikiti huo na kuchimba misingi na mashimo katika eneo hilo.

Duru za Palestina katika mji wa Quds zinatahadharisha kuwa, njama hiyo ya utawala wa Kizayuni inahatarisha usalama wa msikiti wa Al Aqsa na kuta zake na kuna uwezekano wa kuporomoka wakati wowote ule. Duru hizo zimeongeza kuwa kwa sababu hiyohiyo, kuta za eneo la kale la mji wa Quds, nazo pia ziko hatarini kuporomoka.../