Aug 17, 2022 12:10 UTC
  • Mwanamke Saudia afungwa jela miaka 34 kwa ujumbe wa Twitter

Saudi Arabia imemhukumu mwanamke mmoja kifungo cha miaka 34 jela, eti kwa kupatikana na hatia ya kumiliki ukurasa wa Twitter na kusambaza ujumbe unaoukosoa utawala wa Aal-Saud kupitia mtandao huo wa kijamii.

Salma al-Shehab, 34, mama wa watoto wawili wadogo na mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Leeds alikamatwa na vyombo vya usalama vya Saudia Januari mwaka jana, alipokuwa amejerea nyumbani kwa ajili ya likizo, na amekuwa kizuizini tokea wakati huo hadi sasa.

Awali alikuwa amehukumiwa kifungo cha miaka 6 jela, kwa kupatikana na hatia ya eti 'kutumia mitandao ya kijamii kuvuruga nidhamu ya umma na kuhatarisha usalama na uthabiti wa dola.'

Hata hivyo Mahakama ya Rufaa imeangalia upya hukumu hiyo na kumsweka jela miaka 34, mbali na kumpiga marufuku  kusafiri nje ya nchi kwa kipindi cha miaka 34.

Salma Shahab

Kwa mujibu wa gazeti la The Gurdian, mwanaharakati huyo amehukumiwa kifungo hicho kwa shitaka la 'kuwasaidia wale wanaotaka kuibua ghasia katika jamii, na kuyumbisha usalama wa taifa.'

Hukumu hiyo ni muendelezo wa wimbi la ukandamizaji na mbinyo unaofanywa na utawala wa Riyadh ukiongozwa na Mohammed bin Salman, Mrithi wa Ufalme wa Saudia, dhidi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii, wanaharakati na wakosoaji wa utawala huo wa kifalme.

 

Tags