Aug 17, 2022 12:17 UTC
  • Wapalestina wa Gaza wataka kushtakiwa Wazayuni walioua watoto wao

Wakazi wa Ukanda wa Gaza wamefanya maandamano wakitaka kufunguliwa mashitaka utawala wa Kizayuni wa Israel katika mahakama za kimataifa, kwa kuua watoto wa Kipalestina katika eneo hilo ambalo liko chini mzingiro.

Wakazi wa Gaza, familia na jamaa za watoto wa Kipalestina waliouawa shahidi katika mashambulizi ya hivi karibuni ya jeshi katili la utawala haramu wa Israel wamekusanyika katika makaburi ya watoto hao, wakiwa wamebeba mabango yenye jumbe za kulaani jinai za utawala huo pandikizi.

Baadhi ya mabango hayo yalikuwa yameandikwa: Tunataka haki kwa watoto wetu waliouawa shahidi, na Damu za watoto wetu hazitapotea hivi hivi.

Kadhalika waandamanaji hao wametumia maandamano hayo kutangaza uungaji mkono wao kwa mrengo wa muqawama unaopambana dhidi ya utawala ghasibu wa Israel unaotenda jinai za kila aina dhidi ya Wapalestina wasio na ulinzi.

Baadhi ya watoto wa Kipalestina waliouliwa shahidi na Wazayuni huko Gaza

Utawala huo dhalimu ulianzisha  vita dhidi ya Gaza mnamo Agosti 5 na vita hivyo vilimalizika baada ya siku tatu kufuatia upatanishi wa Misri.

Jumla ya watu 49 waliuawa shahidi katika hujuma hiyo ya Israel dhidi ya Gaza katika kipindi hicho wakiwemo watoto 17 huku mamia ya wengine wakijeruhiwa.

Tags