Aug 18, 2022 10:28 UTC
  • Shirika la WHO lapeleka misaada ya kibinadamu Yemen

Shirika la Afya Duniani (WHO) liimepeleka msaada wa dharura wa vifaa vya matibabu ikiwemo maabara kwa lengo la kuinua uwezo wa timu zinazotoa huduma za waathirika wa mafuriko waliopata kiwewe na wahaka.

Hatua hiyo imeelezwa kuwa ni katika kuchukua hatua za dharura kusaidia jamii zilizoathiriwa na mafuriko nchini Yemen. Hiyo ni kwa mujibu wa taarifa iliyoyolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO).

Misaada hiyo ya WHO ni pamoja na wataalamu wabobevu kwenye masuala ya matatizo ya kinafsi, magari 6 ya kubebea wagonjwa na imeunda vituo 34 vya kuchunguza magonjwa kwenye jimbo la Ma’rib ambalo ndio limeathirika zaidi.

Mafuriko hayo yakiwa yamechochewa na mvua kubwa za msimu, yamesambaratisha majimbo kadhaa ya Yemen tangu katikati ya mwezi uliopita, na hadi sasa zaidi ya kaya 35,000 kwenye wilaya 85 za majimbo 16 zimeathirika.

Wakimbizi wa Yemen

 

WHO inasema mafuriko hayo yamesababisha vifo vya takribani watu 77, wakiwemo watoto kwenye majimbo ya Al Bayda, Amran, Dhamar, Hajja, Ma’rib, na Sana’a.

Mwakilishi wa WHO nchini Yemen, Dkt. Adham Rashad amesema, “hatari ya magonjwa yaenezwayo kwa maji na vimelea, ikiwemo Malaria, Kipindupindu na mengine inazidi kuwa kubwa, mvua kubwa zaidi inatarajiwa kuendelea hadi mwisho wa mwezi huu wa Agosti, tumeimarisha hatua zetu kufikia waathirika na kuzuia uwezekano wowote wa mlipuko wa magonjwa haya.”

Yemen inakumbwa na mafuriko katika hali ambayo, nchi hiyo inajongewa na maafa ya kibinadamu kutokana na mashambulio ya anga ya Saudi Arabia na washirikka wake ambayo mbali na kusababisha mauaji yameharibu miundombinu mingi ya nchi hiyo.