Aug 18, 2022 10:30 UTC
  • Ansarullah ya Yemen: Marekani imeua mamilioni ya watu katika maeneo mbalimbali duniani

Mjumbe wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Ansarullah ya Yemen ameashiria jinai za Marekani dhidi ya raia katika maeneo tofauti ya dunia na kusema kuwa, Washington imeua mamilioni ya watu katika pembe tofauti ulimwenguni.

Hizam al-Assad, mjumbe wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Ansarullah ya Yemen ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa jimai wa twitter kwamba, Marekani iliasisiwa miaka 250 iliyopita juuu ya miili na maiti za watu.

Ameongeza kuwa, Marekani imeua mamilioni ya watu kwa ajili ya kujitanua, kudhibiti na kudhoofisha wapinzani na kupora mali na utajiri wa watu, na ikiwa na lengo la kupata uhakika wa matokeo imekuwa na uchochezi wa moja kwa moja katika vita vita vya niaba.

Mashambulio ya kijeshi ya Marekani dhidi ya Iraq, Afghanistan, Vietnam, Japan, kuunga mkono utawala wa Baath wa Iraq katika uchokozi na mashambulio yake dhidi ya Iran, himaya ya Washington kwa utawala wa Saudi Arabia katika mashambulio yake dhidi ya Yemen na kuyasaidia makundi ya kigaidi ni sehemu tu ya jinai za Marekani dhidi ya watu duniani ambapo mamilioni ya watu wameuawa katika matukio hayo ya kinyama.

 

Jinai za Marekani katika maeneo tofauti ya dunia hususan katika mataifa ya Kislamu na eneo la Asia Magharibi yamewashangaza mno akthari ya watu ulimwenguni na kuwaacha wakijiuliza inawezekana vipi serikali ikafanya mauaji na jinai zote hizi na jumuiya za kimataifa zikaiacha na kuichukulia hatua yoyote?