Aug 19, 2022 02:40 UTC
  • Mazungumzo ya vyama; njia ya kuikwamua Iraq katika mgogoro

Rais, Waziri Mkuu na Spika wa Bunge pamoja na vyama kadhaa vya siasa vya nchi hiyo wametoa taarifa wakisisitizia ulazima wa kukomeshwa aina yoyote ile ya mzozo na mvutano katika mitaa na barabara za nchi hiyo.

Aidha wamesisitizia umuhimu wa kufanyika mazungumzo kwa ajili ya kuikwamua nchi hiyo na mgogoro wa sasa unaoikabili. Iraq imeendelea kushuhudia mkwamo wa kisiasa kwa miezi kumi sasa ambao chimbuko lake ni matokeo ya uchaguzi wa Bunge uliofanyika Oktoba mwaka jana 2021. Hakuna mrengo wowote au hata waitifaki wao waliofanikiwa kupata viti vya Bunge ambavyo vinawapa uwezo na mamlaka ya kisheria ya kuteua Rais na Waziri Mkuu. Mkwamo wa sasa wa kisiasa wa Iraq kiini chake ni mambo makuu matatu ambayo ni namna ya kugawa madaraka, ukaidi wa kisiasa wa baadhi ya shakhsia na kupuuzwa kanuni za kisiasa bila kusahau uingiliaji wa kigeni katika masuala ya ndani ya nchi hiyo.

Nchini Iraq Rais anapaswa kutoka katika jamii ya Wakurdi, Waziri Mkuu anachaguliwa miongoni mwa Waislamu wa madhehebu ya Shia huku Spika wa Bunge akiteuliwa kutoka miongoni mwa Waislamu wa Kisuni. Aina hii ya ugavi wa madaraka chimbuko lake ni muundo wa kijamii wa Iraq, ingawa kivitendo hili nalo liimekuwa na changamoto zake. Changamoto kuu ni namna ya kuanisha vyeo vikuu vya madaraka.

Kwa mujibu wa katiba ya Iraq, Rais anachaguliwa na Bunge na anapaswa kupata theluthi mbili ya kura za ndio za Wabunge. Hii ni katika hali ambayo, Waziri Mkuu anapaswa kupata asilimia 50+kura moja ya kura za Wabunge. Hali hii inafanya suala la uundaji wa serikali kutowezekana isipokuwa kwa kuweko muungano wa vyama na mirengo ya kisiasa. Endapo kutakuweko na mgawanyiko mkubwa miongoni mwa makundi na mirengo ya kisiasa nchini Iraq wakati huo ni vigumu na jambo lisilowezekana kwa Rais aliyependekezwa kupata theluthi mbili ya kura au Waziri Mkuu asilimia ya kura za Wabunge kama ilivyoelezwa na katiba.

Mustafa al-Kadhim, Waziri Mkuu wa Iraq

 

Filihali hii ndio anga ambayo imejitokeza nchini Iraq tangu uchaguzi wa Bunge ulipofanyika Oktoba mwaka jana na hivyo kuwa moja ya sababu ya nchi hiyo kutumbukia katika mkwamo mkali wa kisiasa na wa muda mrefu zaidi.

Ukaidi wa kisiasa na kupuuzwa kanuni nazo ni sababu nyingine ambazo zimeitumbukiza Iraq katika mkwamo huu wa kisiasa. Mazingira tajwa ambayo yanahusiana na uundaji wa serikali na mpangilio wa madaraka yanaweka wazi ukweli huu kwamba, itawezekana kuepukana na mkwamo wa kisiasa pale tu kutakapokuweko hali ya kuwa tayari kulegeza kidogo msimamo na kujiepusha na tamaa ya kuhodhi madaraka. Katika mazingira kama hayo itawezekana kuteua watu katika nyadhifa mbalimbali na vyeo muhimu nchini humo kama Rais na Waziri Mkuu.

Pamoja na hayo katika kipindi cha miezi kkumi iliyopita Iraq haijashuhudia hali hiyo tuliotangulia kuitaja, na hiyo inatajwa kuwa sababu kuu ya hali ya sasa ya kisiasa inayokabiliwa nayo Iraq.

Siku ya Jumatano, Waziri Mkuu wa Iraq Mustafa al-Kadhim alitoa taarifa akiyataka makundi na mirengo yote ya kisiasa nchini Iraq ihudhurie mkutano wa kitaifa katika makao ya Waziri Mkuu ili ijadili namna ya kuiondoa Iraq na mgogoro wa sasa wa kisiasa. Mrengo wa Harakati ya al-Sadr ulikataa kuhudhuria mkutano huo.

Bunge la Iraq

 

Uingiliaji wa kigeni nao ni sababu nyingine muhimu inayoelezwa na wajuzi wa mambo kwamba, imechochea na kushadidisha mkwamo wa kisiasa na anga jumla ya kisiasa nchini humo. Baadhi ya mataifa ya eneo na ya nje ya eneo hili la Asia Magharibi yakiwa pamoja na utawala haramu wa Israel yanaridhia hali hii tete ya kisiasa nchini Iraq na katu hayataki kuona kunakuweko Iraq thabiti na imara. Upinzani wao dhidi ya Harakati ya Wananchi ya Hashd al-Shaabi na makundi ya muqawama kwa ujumla ndio sababu kuu ya takwa lao, takwa ambalo linapelekea kuingilia masuala ya ndani ya Iraq hususan katika uundaji wa serikali baada ya uchaguzi wa Oktoba mwaka jana.

Hassan Hanizadeh, mweledi wa masuala ya eneo anasema kuwa: Mbali na madola ya kieneo na ya nje ya eneo kutofurahishwa na uteuzi wa Muhammad Shia al-Sudani kwa ajili ya kuchukua wadhifa wa Waziri Mkuu, mtu ambaye ni Muumini wa Kishia na aliye karibu na mrengo wa Daulat Kanun unaoongizwa na Nouri al-Maliki, kuna vibaraka wa ndani ambao nao wamekuwa na mchango katika kushadidisha mizozo na hitilafu baina ya mirengo ya kisiasa ya nchi hiyo.

Baada ya mkwamo wa kisiasa wa Iraq kuingia katika hatua ya uasi, mikusanyiko ya barabarani na maandamano ambayo yamepelekea pia kushambulia Bunge na kivitendo kufunga njia ya maafikiano ya kisiasa, Mustafa al-Kadhim Waziri Mkuu wa serikali ya sasa ya muda ametangaza kuwa, ili kuutatua mkwamo wa sasa wa kisiasa nchini Iraq kuna haja ya kuweko mazungumzo ya kitaifa. Mkutano huo ulifanyika siku ya Jumatano kwa kuhudhuriwa na wakuu wa vyombo vikuu vitatu vya dola na viongozi wa makundi ya kisiasa ya kitaifa pamoja na mjumbe maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Iraq.

Muqtada al-Sadr, Kiongozi wa Harakati ya al-Sadr ya Iraq

 

Taarifa ya mwisho ya kikao hicho imeeleza kuwa: Waliohudhuria wamekubaliana juu ya kuendelezwa mazungumzo ya kitaifa kwa shabaha ya kupata Ramani ya Njia kwa minajili ya kuupatia ufumbuzi mgogoro wa sasa wa nchi hiyo. Aidha wametaka kukomeshwa aina yoyote ile ya mzozo na mvutano wa barabarani, wa propaganda za kihabari na kisiasa, kama ambavyo wameeleza ulazima wa kulindwa asasi za nchi na kutuliza mijadala sambamba na kujiepusha na vitendo vya uchochezi.

Nukta ya mwisho ni kwamba, licha ya kuwa katika taarifa hiyo kumetiliwa mkazo juu ya ulazima wa kufanyika mazungumzo ya kitaifa, lakini wakati huo huo kufanyika uchaguzi wa mapema wa Bunge, nalo limependekezwa kama utatuzi mwingine wa kuiondoa Iraq katika mkwamo wa sasa ambapo hii inaonyesha kuwa, maslahi ya baadhi ya shakhsia na makundii ya Iraq yapo zaidi katika kuitishwa tena uchaguzi na siyo kufanyika mazungumzo ya kitaifa.

Tags