Aug 19, 2022 04:05 UTC
  • Yemen yaonya kuhusu harakati za kutia shaka za askari wa US, Ufaransa

Bunge la Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen limetadharisha kuhusu harakati na nyendo za kutiliwa shaka za wanajeshi wa Marekani na Ufaransa katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu kusini mwa nchi hiyo ya Kiarabu.

Katika taarifa, Bodi ya Uongozi ya Bunge la Yemen imesema harakati hizo za wanajeshi wa Marekani na Ufaransa ambao ni waungaji mkono wa Kimagharibi kwa vita vya Saudi Arabia dhidi ya Yemen, zinatia wasi wasi mkubwa.

Bunge hilo limeonya kuwa, nyendo hizo ni sehemu ya juhudi za muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudia za kukwamisha utekelezaji wa makubaliano ya usitishaji vita ya Umoja wa Mataifa.

Kadhalika Bodi ya Uongozi ya Bunge la Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen imesema italibebesha dhima 'Baraza la Urais' linaloongozwa na Saudia na Imarati, kwa njama zao chafu ndani na nje ya nchi, na kusisitiza kuwa baraza hilo halina uhalali wowote na wala haliwawakilishi wananchi wa Yemen.

Askari wa Ufaransa nchini Yemen

Wayemen wamekuwa wakisisitiza kuwa, Umoja wa Mataifa na nchi zinazounga mkono kwa hali na mali muungano vamizi dhidi ya Yemen unaoongozwa na Saudi Arabia ni wahusika wa jinai zote za kibinadamu na kimazingira katika nchi hiyo maskini ya Kiarabu.

Mashambulizi yanayoendelea kufanywa na muungano vamizi unaoongozwa na Saudia licha ya kuwepo makubaliano ya usitishaji vita ya UN yanakwamisha juhudi za kurejeshwa amani huko Yemen.  

Tags