Aug 21, 2022 02:45 UTC
  • HAMAS yalaani hatua ya Polisi ya Ujerumani ya kufuatilia kauli ya Abbas kuhusu Holocaust

Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS, imelaani hatua ya maafisa wa Polisi ya Ujerumani ya kuamua kuchunguza matamshi aliyotoa Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina na kusisitiza kuwa hatua hiyo inadhihirisha kuwa si kweli kama Berlin haipendelei upande wowote.

Hivi karibuni, wakati Mahmoud Abbas maarufu kwa lakabu ya Abu Mazin alipotembelea Berlin aliulizwa suali na mwandishi wa habari: "je, una nia ya kuomba radhi kwa shambulio la kigaidi lililofanywa na vikosi vya Wapalestina katika michezo ya Olimpiki miaka 50 iliyopita na kupelekea kuuawa wanamichezo wa Israel?"

Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina alijibu suali hilo kwa kusema: "kama mnataka kuangalia yaliyotokea nyuma, fanyeni hivyo; kuanzia mwaka 1947 hadi sasa, Israel imeshafanya mauaji 50 ya Holocaust katika sehemu 50 za Palestina".

Kwa mujibu wa gazeti la Kijerumani la Frankfurter Allgemeine Zeitung, polisi ya Berlin inaanzisha uchunguzi dhidi ya Abbas kwa sababu ya kuunasibisha utawala wa Kizayuni wa Israel na Holocaust.

Mjumbe wa ofisi ya kisiasa ya Hamas Husam Badran ametoa kauli kuhusiana na uamuzi uliochukuliwa na polisi ya Ujerumani akisisitiza kuwa harakati hiyo inalaani hatua na uamuzi huo.

Image Caption

 

Badran amebainisha kwamba, hatua hiyo ya Ujerumani inaonyesha wazi kuwa wanaojidai kutopendelea upande wowote, katika kadhia ya jinai zinazofanywa na utawala ghasibu wa Israel wanaupendelea upande wa Wazayuni na kukandamiza haki za watu wa Palestina.

Inafaa kuashiria hapa kuwa kamisheni maalumu polisi ya Ujerumani imeanzisha uchunguzi kuhusiana na kauli aliyotoa Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina ya kushabihisha mwenendo wa Israel na Holocaust, yanayotajwa kuwa ni mauaji ya halaiki ya Wayahudi yaliyofanywa na Ujerumani ya Manazi. Uchunguzi huo unaweza kuyafanya matamshi ya Abbas yaonekane kuwa kosa la uhalifu.

Kansela Olaf Scholz wa Ujerumani naye pia ameliingilia suala hilo kwa kuandika ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter kwa lugha tatu za Kiingereza, Kijerumani na Kiebrania akisema: "nimechukizwa na kauli ya tusi ya Rais Mahmoud Abbas wa Palestina; na hasa kwa vile kwetu sisi Wajerumani unasibishaji wa aina yoyote kuhusu Holocaust hauvumiliki na haukubaliki; na mimi ninalaani hatua yoyote ya kujaribu kukanusha jinai ya Holocaust".

Kutokana na kushadidi lawama dhidi yake, Mahmoud Abbas ametoa taarifa iliyotangazwa na shirika la habari la Palestina WAFA akisema, Holocaust ndio jinai ya kutisha zaidi katika historia ya wanadamu ya zama mpya.../

Tags