Sep 04, 2022 02:24 UTC
  • Manowari ya Uturuki yatia nanga katika bandari ya Haifa Palestina inayokaliwa kwa mabavu

Vyombo vya habari vya Kiebrania vimeripoti kuwa manowari ya Uturuki pamoja na meli ya kivita ya kombora ya Marekani zimetia nanga katika bandari ya Haifa kaskazini-magharibi ya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.

Uturuki na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel hivi karibuni zilitangaza kuwa zimerejesha tena kikamilifu na katika hali ya kawaida uhusiano wao wa kidiplomasia. Waziri Mkuu wa muda wa utawala wa Kizayuni Yair Lapid na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu walitangaza rasmi mwishoni mwa mwezi uliopita wa Agosti kwamba uhusiano kati ya pande hizo mbili umerejea katika hali ya kawaida na kwamba hivi karibuni Tel Aviv na Ankara zitateua mabalozi wao.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Fars, Itai Blumenthal, ripota wa televisheni ya Kizayuni ya Kan, ameandika kwenye mtandao wake Twitter kwamba, meli hiyo ya kivita ya Uturuki ilitia nanga kwenye bandari ya Haifa Jumamosi asubuhi.
Mevlut Cavusoglu (kushoto) na Yair Lapid walipokutana Tel Aviv

Blumenthal amesema, kupelekwa manowari hiyo ya Uturuki huko bandari ya Haifa inawezekana ikawa ni sehemu ya operesheni za doria zinazofanywa na vikosi vya Shirika la Kijeshi la NATO, na akabainisha kuwa kuingia na kutia nanga meli za Uturuki katika maji ya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu zilizopewa jina la Israel si jambo la kawaida na wala si kila siku.

Mwandishi huyo wa habari wa televisheni ya Kizayuni ya Kan ameongeza kuwa, manowari hiyo ya Uturuki inaitwa TCG Kemalreis (F-247) na imetia nanga kwenye bandari ya Haifa pamoja na manowari ya makombora ya Marekani iitwayo USS Forrest Sherman (DDG-98).

Uhusiano wa Uturuki na utawala wa Kizayuni wa Israel ulikuwa umedorora na kutawaliwa na mivutano kwa muda wa miaka 12 kufuatia tukio la meli ya Uturuki ya "Mavi Marmara". Mwaka 2010, jeshi la utawala haramu wa Israel lilishambulia meli hiyo ya Msafara wa Uhuru" iliyokuwa imebeba shehena za misaada ya kibinadamu kwa kwa ajili ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza. Raia 10 wa Uturuki miongoni mwa wanaharakati waliokuwemo ndani yake waliuawa katika hujuma hiyo ya jeshi la Kizayuni.../

Tags