Sep 10, 2022 11:37 UTC
  • UNICEF yaitaka serikali ya Taliban ifungue skuli zote za wasichana Afghanistan

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) limeitaka serikali ya Taliban inayotawala Afghanistan izifungue skuli zote za wasichana nchini humo.

Baada ya kuingia madarakani Agosti 15, 2021, kundi la Taliban lilizifunga skuli za wasichana za ngazi ya kati na sekondari kwa lengo la kufanya baadhi ya mageuzi.
Shirika la habari la Shafaqna Afghanistan limeripoti leo kuwa UNICEF imeitaka serikali ya Taliban ifikirie upya maamuzi yake na kuzifungua tena skuli zote za wasichana.
Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika hilo la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, jumla ya wasichana milioni tatu nchini Afghanistan wamekosa kwenda skuli.
Hii ni katika hali ambayo serikali ya Taliban iliunda tume ya kufuatilia suala kufunguliwa tena skuli za wasichana, lakini ripoti kuhusiana na kazi iliyofanywa na tume hiyo haijatolewa hadi sasa.
Viongozi wa Taliban

Baada ya kuingia madarakani nchini Afghanistan, Taliban waliahidi kubadilika zaidi katika suala la kuheshimu haki za binadamu na haki za wanawake ikilinganishwa na kipindi walipokuwa madarakani mwaka 1996-2001. Lakini wananchi wengi wa Afghanistan na jamii ya kimataifa wanaamini kuwa serikali ya kundi hilo imekuwa ikizibana hatua kwa hatua haki za Waafghani hasa wanawake, kwa kuwazuia kurudi maskulini na kutowaruhusu wanawake kufanya kazi katika sekta nyingi serikalini.

Kudhamini haki za msingi za wanawake, kufungua upya skuli zote za wasichana, kuhakikisha ardhi ya Afghanistan haitumiwi dhidi ya nchi zingine, na kuunda serikali pana na jumuishi ni miongoni mwa masharti yaliyotolewa na jamii ya kimataifa kwa ajili ya kuitambua serikali ya Taliban.../

 

Tags