Sep 17, 2022 01:25 UTC
  • Wakuu wa Intelijensia wa Uturuki na Syria wakutana Damascus kuandaa mkutano wa viongozi wa juu wa nchi mbili

Shirika la habari la Reuters limezinukuu duru za Syria na Uturuki na kutangaza kuwa Hakan Faidan, mkuu wa shirikia la intelijensia la Uturuki na mwenzake wa Syria Ali Mamluk wamekutana kwa mazungumzo katika mji mkuu wa Syria Damascus ili kuandaa mazingira ya mkutano wa viongozi wa ngazi ya juu zaidi wa nchi mbili.

Kwa mujibu wa shirika la habari la al-Mayadeen, Reuters, imezinukuu duru nne za Damascus na Ankara na kutangaza kuwa, katika wiki chache zilizopita, wakuu wa mashirika ya Ujasusi ya Uturuki na Syria wamefanya vikao kadhaa mjini Damascus kwa lengo la kuandaa mazingira ya mikutano ya viongozi wa ngazi za juu wa nchi mbili.
Duru za kieneo zimeripoti kuwa, uhusiano wa Uturuki na Syria umeanza kuboreka na unaendelea kupiga hatua ili kufikia kwenye anga ya maelewano.
Kuhusiana na suala hilo, afisa mmoja mwandamizi na duru moja ya kiusalama ya Uturuki wameripoti kuwa Russia inataka Syria na Uturuki zisuluhishe tofauti zao na kufikia makubaliano yenye manufaa kwa pande zote mbili. Lakini moja ya changamoto kubwa ni msimamo wa Uturuki wa kutaka wapinzani wa Syria washirikishwe katika mazungumzo na serikali ya Damascus.

Kwa upande mwingine, tovuti ya chaneli ya televisheni ya Halk TV, ambayo inaipinga serikali ya Uturuki, ilifichua siku ya Alhamisi taarifa zaidi za mkutano wa siri wa wakuu wa mashirika ya ujasusi ya Uturuki na Syria, na kutangaza kuwa, katika mkutano huo, pande mbili zilijadili pamoja na mambo mengine suala la wakimbizi, ambalo ni moja wa kadhia muhimui kwa Uturuki, hasa kwa kuzingatia kukaribia kwa uchaguzi mkuu ujao wa nchi hiyo.

Madai hayo ya shirika la habari la Reuters yametolewa wakati Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu akiwa ametangaza hapo awali kwamba, mashirika ya ujasusi ya Uturuki na Syria yanawasiliana.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki ameeleza pia kwamba alifanya mazungumzo mafupi na Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria Faisal al-Maqdad pembeni ya mkutano wa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote.../

Tags