Sep 17, 2022 01:25 UTC
  • Mwanachuoni Msuni wa Iraq: Tunaona fakhari kuwa wenyeji wa mazuwari wa Imam Husain

Mkuu wa Jumuiya ya Ahlu Sunna Waljamaa ya Iraq amesema kuwa, hivi sasa Waislamu wa Iraq wanaonesha kivitendo mfano bora kabisa wa ukarimu kwa kuwahudumia kwa moyo mmoja wafanyaziara wa Imam Husain AS kutoka kila kona ya dunia.

Leo Jumamosi mwezi 20 Mfunguo Tano Safar 1444 Hijria yanafikia kileleni maadhimisho ya Arubaini ya Imam Husain AS ambayo kwa Afrika Mashariki ni maarufu kwa jina la Hussein Day.

Waislamu na hasa wafuasi wa Ahlul Bait wa Mtume Muhammad SAW wamemiminika kwa mamilioni katika jangwa la Karbala, kusini mwa Iraq hivi sasa kwa ajili ya maadhimisho ya Arubaini ya Imam Husain AS.

Shirika la habari la FARS limemnukuu Sheikh Khalid al Malaa, Mkuu wa Jumuiya ya Ahlus Sunna Waljamaa ya Iraq akielezea hisia zake kutokana na mamilioni ya wafanyaziara wanaotembea kwa miguu katika maadhimisho ya Arubaini ya Imam Husain AS kusisisiza kuwa, kadhia ya Imam Husain AS imebebwa na hisia kali, na chochote kinachohusiana na Imam Husain AS ni cha kipekee na kinakuwa na hisia kali kutokana yaliyotokea kwenye mapambano yake katika jangwa la Karbala mwaka 61 Hijria.

Sheikh Khalid al Malaa, Mkuu wa Jumuiya ya Ahlus Sunna Waljamaa ya Iraq

 

Mwanachuoni huyo mkubwa wa Kisuni wa Iraq pia amesema, ni fakhari kubwa sana kwetu kuona tunawahudumia wafanyaziara ya Arubaini ya Imam Husain AS. Siku hizi zote, wananchi wa Iraq wamedhihirisha ukarimu wao kwa kiwango cha juu mno na kwa sura ya kipekee kwa sababu ukarimu unaotokana na mapambano ya Karbala ya Imam Husain AS.

Amesema, kila mmoja anapaswa kushirikiana na mwenzake hivi sasa kuhakikisha anatoa mchango wake katika kuwatumikia wageni wa Imam Husain AS. 

Aidha amesema, ziara ya Arubaini ya Imam Husain AS ni utekelezaji wa kivitendo wa umoja na mshikamano katika safu za Waislamu wote wa Kishia na Kisuni na hayo ndiyo yanayotakiwa na Mwenyezi Mungu pamoja na Mtume Wake na Ahlul Bait wake.

Tags