Sep 19, 2022 07:14 UTC
  • Wafanyaziara milioni 1 na nusu watembelea Samarra Iraq baada ya Arubaini

Mji wa Samarra wenye haram mbili tukufu za Maimam wa Ahlul Bayt wa Bwana Mtume Muhammad SAW umeshuhudia wimbi kubwa la wafanyaziara waliolekea mjini humo baada ya kushiriki kwenye Arubaini ya Imam Husain AS huko Najaf na Karbala nchini Iraq.

Taarifa kutoka nchini Iraq zinasema kuwa, zaidi ya wafanyaziara milioni 1 na laki tano wameelekea Samarra katika mkoa wa Salahuddin huko Iraq kwa ajili ya kufanya ziara katika haram mbili za Imam Hadi na Imam Hassan Askari AS ambao ni Maimamu wa 10 na 11 katika kizazi kitoharifu cha Bwana Mtume Muhammad SAW.

Kwa mujibu wa ripoti ya leo Jumatatu ya Middle East News, Muhammad Hussein al Minwari, afisa wa vyombo vya habari vya haram hizo mbili za Samarra ametangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, ziara za wimbi hilo kubwa la mamia ya maelfu ya wapenzi wa Ahlul Bayt AS imefanyika kwa ushirikiano kabili wa taasisi za kulinda usalama za ndani ya Iraq.

Mji wa Samarra nchini Iraq

 

Ameongeza kuwa, wasimamiaji wa masuala ya haram hizo mbili wameandaa mazingira mazuri ya usafiri na huduma nyinginezo zote kwa ajili ya watu wanaofanya ziara kwenye haram hizo.

Amesema, huenda idadi ya wafanyaziara kutoka nje ya Iraq ikaongezeka sana katika mji huo wa Samarra.

Inafaa kukumbusha hapa kwamba, hadi juzi Jumamosi, zaidi ya wafanyaziara milioni moja walikuwa wameshiriki kwenye maadhimisho ya Arubaini ya Imam Husain AS nchini Iraq. Sehemu kubwa ya wafanyaziara hao wa kigeni ni kutoka nchini Iran.

Tags