Sep 23, 2022 02:43 UTC
  • Hamas: Kuhamishiwa Quds ubalozi wa Uingereza hakubadili ukweli wa mambo

Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) ameashiria hatua ya Uingereza eti ya kutangaza nia yake ya kuuhamishia ubalozi wake huko Quds na kueleza kuwa: hatua hiyo haibadili kivyovyote uhakika wa kihistoria.

Gazeti la Telegraph la Uingereza limezinukuu duru za kuaminika na kuripoti kuwa, katika mazungumzo kati yake na Yair Lapid Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni, Liz Truss Waziri Mkuu wa Uingereza amegusia uwezekano wa nchi hiyo kuhamishia ubalozi wake huko Quds. 

Waziri Mkuu wa Uingereza, Liz Truss 

Akizungumza jana Alhamisi na shirika la habari la Shehab, Abdul Latif al Qanou Msemaji wa harakati ya Hamas alieleza kuwa, nia ya Uingereza ya kutaka kuhamishia ubalozi wake huko Quds inadhihirisha upendeleo wa wazi kwa Maghasibu wa Kizayuni lakini kitendo hicho hakiwezi kubadili  kivyovyote uhakika wa kihistoria.   

Al Qanou ameongeza kuwa: Uingereza siku zote inawaunga mkono maghasibu wa Kizayuni wanaoikalia kwa mabavu Quds Tukufu; na nchi hiyo ndiyo iliyowaahidi Wazayuni ardhi ya Wapalestina; kwa hiy kuhamishiwa ubalozi huo pia kunafanyika katika fremu ya kuendeleza uadui na chokochoko dhidi ya matukufu ya Kiislamu na Kikristo.  

Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) amesema: Quds ni ardhi iliyoghusubiwa na kukaliwa kwa mabavu na ni haki ya wananchi wa Palestina. Hatua hiyo ya Uingereza inamaanisha kuwa bega kwa bega na utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi wa Palestina.