Sep 24, 2022 12:35 UTC
  • Kiongozi wa HAMAS aiomba tena Saudia iwaachie huru Wapalestina iliowaweka gerezani

Mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS ametaka Wapalestina wanaoshikiliwa kwenye jela za Saudi Arabia waachiliwe huru.

Wapalestina wapatao 60, akiwemo Muhammad Al-Khadhri, mwanachama mwandamizi wa harakati hiyo, na mwanawe Hani wanashikiliwa katika jela za Saudia.
 
Kwa mujibu wa tovuti ya habari ya Al ahd, Ismail Haniya, mkuu wa ofisi ya kisiasa ya harakati ya Hamas, amemtaka Mfalme Salman bin Abdulaziz wa Saudi Arabia na Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa nchi hiyo Mohammed bin Salman wawaachilie huru Wapalestina wote waliowekwa gerezani nchini humo.
Mfalme Salman (kushoto) na mwanawe Mohammad bin Salman

Hivi karibuni, Khalid Mash'al, mkuu wa harakati ya Hamas nje ya nchi, alifanya mahojiano na chaneli ya televisheni ya Al Jazeera kuzungumzia kufungwa kwa baadhi ya wanachama wa harakati hiyo, akiwemo mwakilishi wake nchini Saudi Arabia, Muhammad Al-Khadhri, na akasema, wanachama hao wa Hamas wanapewa adhabu za mateso ya kutisha.

 
Katika mahojiano hayo na Aljazeera, Mash'al alihoji, Wapalestina wanaozuiliwa Saudi Arabia wanateswa kwa manufaa ya nani na wanashtakiwa kwa sababu na kosa gani?
 
Kabla ya hapo pia, mashirika ya kimataifa ya masuala ya sheria yalilaani kuwekwa kizuizini Wapalestina hao nchini Saudi Arabia na yakatangaza kuwa kesi za watu hao si za haki na zimeendeshwa bila kuwepo mashtaka wala sababu zozote zinazokubalika kisheria.../