Sep 25, 2022 02:43 UTC
  • Taasisi ya Kimataifa ya Quds: Msikiti wa al-Aqswa unakabiliwa na hatari kubwa

Taasisi ya Kimataifa ya Quds imetahadharisha kuhusiana na hatari zinazoukabili msikitii wa al-Aqswa kibla cha kwanza cha Waislamu na kuwataka Maulamaa wa Umma wa Kiislamu kujitokeza na kuukabiliana na njama za maadui dhidi ya eneo hilo takatifu.

Taarifa iliytolewa na taasisi hiyo imetahadharisha kuwa, msikiti mtakatifu wa al-Aqswa unakabiliwa na hatari na njama nyingi tofauti kama uvamizi wa kila mara wa walowezi wa Kizayuni, uchimbaji mashimo na njia za chini kwa chini kuelekea katika msikiti huo na mipango michafu dhidi ya msikiti huo kama kubadilisha utambulisho wake wa asili au njama za kutaka kuubomoa msikiti huo.

Taasisi ya Kimataifa ya Quds imesisitiza kuwa, Maulamaa wa Umma wa kiislamu wanapaswa kujitokeza na kukabiliana na njama hizi chafu za Wazayuni dhidi ya msikiti mtakatifu wa al-Aqswa.

Walowezi wa Kiyahudi wakivamia msikiti wa al-Aqswa

 

Indhari hiyo inatolewa katika hali ambayo, walowezi wa Kizayuni wamekuwa wakiuvamia mara kwa mara msikiti wa al-Aqswa huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu na kuuvunjia heshima msikiti huo mtakatifu.

Katika miezi ya hivi karibuni vitendo vya hujuma na uvamizi wa walowezi wa Kizayuni katika maeneo ya Wapalestina hususan katika Msikiti wa al-Aqswa vimeongezeka mno.

Utawala wa Kizayuni ambao unaungwa mkono kikamilifu na Marekani katika hatua zake hizo haramu umedhamiria kubadilisha muundo wa kijiografia na kidemografia wa maeneo ya Palestina; ili kuyazayunisha maeneo hayo na kuhakikisha unazihodhi na kuzidhibiti kikamilifu ardhi za Wapalestina.