Sep 26, 2022 03:35 UTC
  • Pakistan yapinga tena wazo la kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel

Serikali ya Pakistan kwa mara nyingine tena imepinga wazo la kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel kufuatia uchochezi wa baadhi ya tawala za Kiarabu zenye fikra mgando za kuitaka ifuate mkondo huo.

 Hadi hivi sasa, Pakistan haijautambua utawala haramu wa Kizayuni wa Israel na daima imekuwa ikisisitiza kwamba, kuwaunga mkono wananchi madhulumu wa Palestina dhidi ya utawala huo ghasibu ni msingi na dira inayoainisha siasa na sera zake za nje.

Serikali ya Islamabad kila mara imekuwa ikisisitiza kuwa, serikali na wananchi wa Pakistan wataendelea kuwaunga mkono wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina na mapambano yao ya kupata haki ya kujitawala na kujiamulia mustakabali wao.

Shirika la Habari la Mehr limeripoti kuwa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan, Bilawal Bhutto Zardari, amekanusha kuwa na nia nchi yake ya kuanzisha aina yoyote ile ya uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel na  kusisitiza kwamba, msimamo wa Pakistan kuhusu suala la Palestina uko wazi kabisa na haujabadilika.
 Bilawal Bhutto Zardari

Zardari ameyasema hayo katika mkutano na waandishi wa habari pembezoni mwa Mkutano Mkuu wa 77 wa Umoja wa Mataifa mjini New York.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan ameongeza kuwa, katika taarifa iliyotoa Alkhamisi iliyopita, ofisi yake ilikanusha tuhuma ya kutaka kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel na ikasisitiza kuwa masuala kama hayo hayana uhusiano wowote na serikali ya Pakistan.
Kabla ya hapo, vyombo vya habari vya utawala wa Kizayuni vilidai kuwa, mwaka 2021 maafisa wa Pakistan walifanya safari katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu kwa lengo la kufanikisha mpango wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala huo ghasibu, lakini serikali ya Islamabad imekanusha kufanyika safari hiyo.../

 

Tags