Sep 27, 2022 04:45 UTC
  • HAMAS: Taifa la Palestina litapata ushindi katika vita vyake na utawala haramu wa Israel

Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiiislamu ya Palestina HAMAS amesema kuwa, taifa la Palestina ndilo litakaloibuka na ushindi katika vita na utawala ghasibu wa israel.

Hazim Qassim, msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiiislamu ya Palestina HAMAS amesisitiza kuwa, himaya, uungaji mkono, muqawama na kusimama kidete taifa la Palestina ni mambo ambayo mwisho wa siku yatalifanya liibuke na ushindi mbele ya utawala vamizi wa Israel unaoungwa mkono kwa hali na mali na madola ya Magharibi.

Kiongozi huyo wa Hamas ameeleza kuwa, chaguo pekee la kuikomboa Palestina na kuiondoa katika makucha ya Wazayuni wamwagaji damu ni kudumisha muqawama na mapambano dhidi ya maadui hao wanaotenda jinai kila uchao dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina.

 

Wito huo unatolewa sambamba na kushadidi hujuma na uvamizi wa walowezi wa Kiyahudi dhidi ya msikiti mtakatifu wa al-Aqswa kibla cha kwanza cha Waislamu. Hujuma hizo zinakwenda sambamba na kuimarishwa ulinzi na usalama sanjari na kuanza maadhimisho ya sikukuu za Kiyahudi.

Katika miezi ya hivi karibuni vitendo vya hujuma na uvamizi wa walowezi wa Kizayuni katika maeneo ya Wapalestina hususan katika Msikiti wa al-Aqswa vimeongezeka mno.

Vitendo vya kuyavunjia heshima matukufu ya Kiislamu huko Palestina vinafanyika katika hali ambayo, viongozi wa nchi za Kiarabu na jamii ya kimataifa wameendelea kunyamaza kimya na kutochukua hatua zozote za maana za kukabiliana na vitendo hivyo vinavyokinzana na utu na ubinadamu.

Tags