Sep 27, 2022 10:15 UTC
  • Ansarullah: Israel imetiwa kiwewe na makombora ya balestiki ya masafa marefu ya Yemen

Mjumbe wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Ansarullah ya Yemen amesema kuwa, nchi yake hivi sasa inamiliki makombora ya balestiki ya masafa marefu, suala ambalo limeutia kiwewe utawala wa Kizayuni wa Israel.

Televisheni ya al Mayadeen imeripoti habari hiyo na kumnukuu Ali al-Qahum akisisitiza kuwa, makombora hayo ya balestiki ya masafa marefu yanaweza kufika kwenye ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni na yamewatia kiwewe viongozi wa utawala wa Kizayuni wa Israel.

Ameongeza kwa kusema: "Sisi tumekubali kusimamisha vita na wavamizi wa Yemen kwa sababu yanatugusa sana masuala ya kibinadamu. Tunaamini kuwa hatua hiyo itapelekea kuacha kuzingirwa Yemen, ingawa madola vamizi yanaendelea kushikilia hatua za kijeshi."

Ali al Qahum

 

Mjumbe huyo wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Ansarullah ya Yemen pia amesema, nchi zinazoshiriki katika muungano vamizi unaofanya jinai kubwa dhidi ya wananchi wa Yemen, zinawaunga mkono magaidi wa al Qaida, suala ambalo linazidi kuthibitisha uadui wao kwa taifa hilo la Waislamu.

Aidha amesema, makubaliano ya kusimamisha vita ni mlango wa kuingilia kwenye utatuzi wa kisiasa wa mgogoro wa Yemen, lakini inasikitisha kuona kuwa madola vamizi yanayoongozwa na Saudi Arabia, yanafanya njama za kuyatia nguvu magenge ya kigaidi ya Daesh na al Qaida. Hata hivyo amesema, wananchi Waislamu wa Yemen wataendelea kusimama kidete kuilinda nchi yao.

Ni vyema tuseme hapa kwamba, tarehe pili Agosti mwaka huu, Umoja wa Mataifa uliongeza muda wa miezi miwili makubaliano ya usimamishaji vita huko Yemen. Makubaliano hayo ya muda yalifikiwa tarehe pili Aprili mwaka huu kwa upatanishi wa Umoja wa Mataifa.