Sep 28, 2022 09:02 UTC
  • Usitishaji usiositishwa wa vita vya Yemen

Sambamba na kukaribia tarehe Pili Oktoba, siku utakapokamilika muhula wa miezi miwili wa usitishaji vita nchini Yemen, zoezi la kusimamisha mapigano katika vita vya nchi hiyo ambalo lilianza rasmi tarehe Pili Juni mwaka huu, litakuwa limekamilisha duru yake ya pili.

Mbali na Timothy Linderking, ambaye ni mjumbe wake maalumu katika masuala ya Yemen, Marekani imemtumia pia mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Yemen, Hans Grundberg, ili kuandaa mazingira ya kurefusha tena, na ikiwezekana kwa muda mrefu zaidi usitishaji vita huo; ili kwa kufanya hivyo, isiwe na wasiwasi tena wa kusafirisha bidhaa za nishati kutoka eneo la Ghuba ya Uajemi na Langobahari la kistratejia la Bab Al Mandab kuelekea masoko ya nishati kwa ajili ya matumizi hasa katika nchi za Magharibi; na kwa njia hiyo, kuzuia kuongezeka bei ya nishati, hasa kutokana na kukaribia uchaguzi wa bunge la nchi hiyo unaotazamiwa kufanyika mwezi Novemba.
Hans Grundberg, mjumbe maalumu wa UN Yemen

Hii inamaanisha kwamba, tokea hapo awali, lengo na sababu ya Marekani kuunga mkono usitishaji vita huko Yemen haikuwa ni kuguswa na hali mbaya ya kibinadamu, wala kufanikisha upelekaji huduma na misaada nchini humo; bali ni kuhakikisha vituo vya mafuta vya Saudi Arabia vinasalimika na mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani za vikosi vya ulinzi vya Yemen. Kwa sababu, kama msimamo wa Washington ungekuwa umetokana na sababu za kiutu, ingefuatilia usitishaji vita nchini Yemen kabla mtikisiko wa vita vya Ukraine haujateteresha masoko ya nishati na matumizi yake katika nchi za Magharibi. Na baada ya hapo, ingeishinikiza pia Saudi Arabia ikomeshe mwenendo wake wa kukiuka mara kwa mara usitishaji vita huo. Lakini baada ya kusitishwa mapigano, Marekani iliondoa mashinikizo iliyokuwa imeiwekea Saudia, ili kwa upande mmoja, kuifanya ihalifu bila ya hofu ahadi ilizowekeana na Russia katika jumuiya ya OPEC+; na kwa upande mwingine, kupata njia pia ya kuilazimisha iongeze uzalishaji wake wa mafuta; na mkabala wake, Riyadh nayo kupata ujasiri na uthubutu wa kuendelea kutekeleza bila hofu malengo ya kijeshi inayofuatilia nchini Yemen.

Ukiukaji wa usitishaji vita unofanywa na Saudi Arabia na waitifaki wake yemen

Kujitokeza na kuendelea kwa hali hii kumeifanya serikali na wananchi wa Yemen wawe na shaka na hatihati ya kurefusha tena usitishaji vita; kwa sababu kiuhalisia, hawajaona mabadiliko yoyote katika mwenendo na muamala wa madola vamizi; na mkabala wake, kutokana na wao kufungika mikono kwa kisingizio cha usitishaji vita, hawawezi kufanya chochote ili kujibu uchokozi na ukiukaji wa mara kwa mara wa usitishaji mapigano unaofanywa na madola hayo. Na ndiyo kusema kuwa, usitishaji huo wa mapigano ama umeyanufaisha madola vamizi kwa kuweza kuimarisha kuwepo kwao kijeshi katika maeneo ya Yemen yanayoyakalia kwa mabavu; au umeyanufaisha madola ya Magharibi, ambayo yamefanikiwa kuzuia kupanda tena bei ya nishati, na vilevile kwa kuyatumia madola vamizi ya Saudia na Imarati pamoja na vibaraka wao, yanaweza kununua kwa bei rahisi rasilimali za mafuta na gesi ya Yemen zinazoporwa na makampuni ya mafuta na gesi ya nchi hizo.

Akiba ya mafuta ya Yemen ni takriban mapipa bilioni 11.950; na hifadhi yote ya gesi ya nchi hiyo ni karibu futi za ujazo trilioni 18.283. Waziri wa Mafuta wa Serikali ya Wokovu wa Kitaifa wa Yemen ametangaza kuwa, mapato ya mafuta ya nchi hiyo yaliyoporwa kuanzia mwaka  2018 hadi Julai mwaka huu ni jumla ya dola bilioni 9 na milioni 500, ambazo, zikijumuishwa na rasilimali za mafuta zilizoporwa kabla na baada ya kipindi hicho, bila shaka kiwango kamili cha thamani ya mafuta hayo ni kikubwa zaidi mara kadhaa.
Hata kama takwimu kuhusu kiwango cha rasilimali ya gesi ya Yemen iliyoporwa hazijatolewa, lakini kwa kuzingatia kuwa mradi wa gesi asilia ni moja ya miradi mikubwa zaidi ya kiuchumi ya Yemen, ilikuwa ikikadiriwa kwamba, ndani ya muda wa miaka 30, pato la rasilimali hiyo lingekuwa karibu dola bilioni 30 hadi 50. Kwa hiyo, kama thamani ya rasilimali ya gesi ya Yemen iliyoporwa si kubwa zaidi kuliko ya mafuta yake yaliyoporwa, basi si kidogo kuliko hiyo. Kwa kuzingatia kuwa hata kabla ya uvamizi wa Saudia na Imarati, Yemen ilikuwa nchi masikini na yenye maendeleo duni, hivi sasa imekuwa masikini zaidi. Mwenendo wa ustawi wa nchi hiyo umerudishwa nyuma kwa miongo kadhaa; na muhimu zaidi kuliko yote,Yemen imepata hasara kubwa ya mapato yanayotokana na akiba yake ya mafuta na gesi, mbali na roho za makumi ya maelfu ya watu ambao wameuawa na kujeruhiwa.
Takwimu zilizotolewa zinaonyesha kuwa, katika miaka saba tu ya kwanza ya uvamizi wa kijeshi uliofanywa dhidi ya Yemen, taasisi 604,000 za utoaji huduma, karibu nyumba laki sita; taasisi 182 za vyuo vikuu; misikiti 1,612; vituo 375 vya utalii, hospitali na zahanati 410; skuli na vituo vya mafunzo 1,214; viwanja na vituo vya michezo 139 na maeneo 9,721 ya kilimo yameharibiwa kutokana na athari za moja kwa moja za mashambulio ya anga yaliyofanywa na madola vamizi. 
Ndege za kivita za Magharibi zinazotumiwa katika vita dhidi ya Yemen

Kwa kuzingatia kuwa ndege zote zilizotumiwa katika mashambulio hayo zimetengenezwa Marekani au Ulaya, kwa hivyo serikali za Magharibi nazo pia zinahusika na zimeshiriki katika jinai za kivita zilizofanywa na majeshi vamizi ya Saudia na Imarati. Katika muda wa miezi minne ya usitishaji vita, Serikali ya Wokovu wa Kitaifa ya Yemen imetoa fursa kwa madola vamizi na waungaji mkono wao wa Magharibi kurekebisha mtazamo wao, lakini kwa kuzingatia kwamba hakuna mabadiliko yoyote yaliyofanywa na madola hayo, sasa imeamua kwa mara nyingine tena kupigania haki yake ya kujihami.../