Sep 28, 2022 10:45 UTC
  • HAMAS: Mapambano yataendelea hadi zitakapokombolewa ardhi zote za Palestina

Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema kuwa, mapambano katika mji wa Jenin wa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan yataendelea hadi utakaposhindwa kikamifu utawala wa Kizayuni na kutimuliwa katika ardhi zote za Palestina.

Duru rasmi za Palestina zimetangaza kuwa, kwa uchache Wapalestina watatu wameuawa shahidi na wengine 9 wamejeruhiwa baada ya wanajeshi katili wa utawala wa Kizayuni kuuvamia mji wa Jenin wa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Msemaji wa HAMAS, Hazem Qassem amesema hayo kuonesha hisia zake kuhusu mapigano yanayoendelea baina ya wanamapambano wa Palestina na wanajeshi dhalimu wa Israel na kuongeza kuwa, mji wa Jenin utaendelea na mapambano yake hadi Wazayuni watakapotimuliwa katika ardhi zote za Palestina.

Amesema, jinai za utawala wa Kizayuni katika mji wa Jenin ni muendelezo wa vitendo vya kigaidi vya utawala huo lakini kamwe hautoweza kuzima mapambano ya wananchi wa mji wa Jenin.

Msemaji wa HAMAS, Hazem Qassem

 

Katika matamshi yake mengine, Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amelaani vikali hujuma na uvamizi unaoendelea wa wanajeshi wa Israel na walowezi wa Kiyahudi katika Msikiti mtakatifu wa al-Aqsa ambao ni Kibla cha Kwanza cha Waislamu kilichoko kwenye mji wa Quds unaokaliwa kwa mabavu na Wazayuni.

Amesema, hatua ya Wazayuni ya kuuvamia msikiti wa al Aqsa ni kuyavunjia heshima matukufu ya Kiislamu na kunaweza kuripua ghadhabu za umma wa Kiislamu zisizoweza kudhibitika.

Kabla ya hapo, Dk. Mahmoud al-Zahar, mjumbe mwandamizi wa Ofisi ya Kisiasa ya HAMAS alikuwa amesema kuwa, utawala haramu wa Israel unatumia vibaya udhaifu uliogubika ulimwengu wa Kiarabu na hivyo kuudhibiti mji wa Beitul-Muqaddas na Msikiti mtakatifu wa al-Aqsa.

Tags