Sep 28, 2022 13:53 UTC
  • Sayyid Abdul Malik Badruddin al-Houthi
    Sayyid Abdul Malik Badruddin al-Houthi

Kiongozi wa harakati ya Ansarullah ya Yemen ameleza jinsi ujumbe wa Mtume wa Mwenyezi Mungu, Muhammad (SAW) unavyogusa na kuzungumzia kila kitu na kusema kuwa, kuelewa umuhimu na ukubwa wa ujumbe wa Mtume wa Mwenyezi Mungu kuna umuhimu na thamani kubwa kwa Umma wa kiislamu.

Sayyid Abdul Malik Badruddin al-Houthi, ameyasema hayo leo (Jumatano) katika mkutano wa mwaka wa wanazuoni wa Yemen wakati wa kukumbuka tukio la Hijra na kuhama Mtume Muuhammad (SAW) kutoka Makka hadi Madina.

Kiongozi wa Ansarullah amesema: "Wanazuoni wa teolojia wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika Umma wetu, na kufanya kazi ya kunyanyua juu Umma wa Kiislamu."

Sayyid Abdul Malik al-Houthi amesema, Mtume (saw) aliwaslilisha mfumo kamili na wenye mlingano kwa ajili ya kunyanyua juu imani na maadili mema na alikuja na ujumbe wa Mwenyezi Mungu unaoweza kutatua matatizo yote ya kisiasa na kijamii ya Umma.

Al-Houthi ameongeza kwa: "Kuna umuhimu wa kukabiliana na juhudi za maadui za kutaka kuipotosha jamii na vijana wetu; na kadiri adui anavyozidisha mashambulizi dhidi ya Umma, ndivyo majukumu ya wasomi ya kukabiliana na mashambulizi hayo yanayovyokuwa makubwa zaidi." 

Kiongozi wa harakati ya Ansarullah amesema: Ni muhimu kutoa miongozo ya Qur'ani kama suluhisho la matatizo ya Umma, na vilevile kutoa maelelzo na ufafanuzi kuhusu miongozo hiyo.

Mkutano wa kila mwaka wa wanazuoni wa Yemen

Baada ya hotuba ya Sayyid Abdul Malik al Houthi, washiriki katika mkutano wa kila mwaka wa maulamaa wa Yemen wameutaka muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia kuheshimu usitishahji wa vita, kusitisha uchokozi, kuondoa mzingiro dhidi ya taifa la Yemen na kutumia fursa hiyo kwa ajili ya kujenga amani ya kiadilifu. Vilevile wamelaani hatua yoyote ya kuanzisha uhusiano wa kawaida baina ya nchi za Kiarabu na utawala haramu wa Israel.