Sep 29, 2022 02:23 UTC
  • Ziad al Nakhala:  Jinai za utawala wa Kizayuni Ukingo wa Magharibi hazitasalia bila ya jibu

Katibu Mkuu wa harakati ya Jihad Islami ya Palestina amesisitiza kuwa jinai za utawala wa Kizayuni huko Jenin katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan hazitaachwa hivi hivi bila ya jibu.

Wanajeshi wa utawala haramu wa Kizayuni kila siku hushambulia maeneo mbalimbali katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan kwa visingizio mbalimbali na kisha kuwauwa shahidi, kuwajeruhi na kuwatia mbaroni raia wa Palestina.  

Ziad al Nakhala amebainisha kuwa: tutatekeleza jukumu letu la  kujibu jinai hizo za utawala wa Kizayuni. Al Nakhala ameongeza kuwa, jinai zinazotekelezwa adui katika mji wa Jenin hazitufanyi tunyamaze kimya na haziwezi kutuzuia kuchukua hatua kukabiliana nazo. 

Duru za Palestina mapema jana ziliashiria uvamizi wa wanajeshi wa Kizayuni katika kambi ya wakimbizi ya Jenin katika Ukingo wa Magharibi wa mto Jordan na kuripoti juu ya kujiri mapigano makali ya silaha kati ya wanamapambano wa Palestina na Wazayuni katika eneo hilo. 

Duru za ndani ya Palestina pia zilitangaza kuwa kundi la askari jeshi maalumu wa jeshi la Israel waliizingira nyumba ya Shahidi Ra'ad Hazim katika mji wa Jenin; mwanamapambano wa Kipalestina aliyetekeleza oparesheni ya kufa shahidi huko Tel Aviv. 

 

Tags