Sep 30, 2022 01:01 UTC
  • Kuimarishwa nafasi ya watoto wa Mfalme Salman katika utawala wa kiukoo wa Saudi Arabia

Mfalme wa Saudi Arabia amemteua Muhammad bin Salman, mrithi wa kiti cha ufalme na mwanaye, kuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo. Pia, Mfalme Salman amemteua mwanaye mwingine, Khalid bin Salman, kuwa Waziri wa Ulinzi.

Mabadiliko hayo yaliyofanyika katika safu ya juu ya utawala wa Saudia yanajumuisha nukta kadhaa za kuzingatiwa:

Kwanza ni kwamba, katika mabadiliko hayo, nafasi ya watoto wa Mfalme Salman imeongezeka katika muundo wa madaraka wa Saudia. Muhammed bin Salman, ambaye ni mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia, ameteuliwa kuwa Waziri Mkuu na mkuu wa Baraza la Mawaziri, nafasi ambayo hapo awali ilikuwa ikishikiliwa na mfalme wa nchi hiyo, na inahesabiwa kuwa wadhifa wa juu zaidi katika muundo wa madaraka nchini Saudi Arabia. Vilevile Khalid bin Salman ameteuliwa kuwa Waziri wa Ulinzi wa Saudia, nafasi ambayo awali ilikuwa ikishikiliwa na Muhammad bin Salman. Kwa maneno mengine ni kwamba, kwa mabadiliko hayo, nafasi ya watoto wa Abdul Aziz madarakani imepungua, na Saudi Arabia sasa amekamatwa sawasawa na waatoto wa Mfalme Salman.

Mabadiliko hayo yamefanyika kwa mujibu wa matakwa ya Muhammad bin Salman. Katika miaka saba iliyopita Bin Salman alikwea kwa kasi ya kupindukia ngazi za madaraka ya juu ya Saudi Arabia kiasi ambacho ni nadra sana kushuhudiwa kwa mtu yeyote mwingine nchini humo. Alikuwa waziri wa ulinzi akiwa na umri wa miaka 30, na naibu mrithi wa ufalme wa Saudia akiwa na umri wa miaka 31. Bin Salman aliteuliwa na baba yake kuwa mrithi kamili wa ufalme akiwa na umri wa miaka 32. Sasa amechukua nafasi na cheo cha juu zaidi cha Waziri Mkuu na kusimamia baraza la mawaziri. 

Bin Salman

Hii ina maana kwamba, uzee wa Mfalme Salman, ambaye ana umri wa miaka 87, umefungua njia ya kutimizwa uchu wa madaraka wa Muhammad bin Salman na kuhamishiwa madaraka kwa watoto wa Salman. Kuhusu mabadiliko hayo mapya, mmoja wa maafisa wa serikali ya Saudia anasema kuwa, nafasi mpya ya Muhammad bin Salman kama mkuu wa Baraza la Mawaziri inaendana na mchakato wa kumpa majukumu ya kifalme, ikiwa ni pamoja na kumuwakilisha mfalme katika safari za nje, na kuongoza mikutano ya kilele inayoandaliwa na Saudi Arabia.

Katika upande mwingine wachunguzi wa mambo wanasema, si sadfa kwa Muhammad bin Salman kuteuliwa kuwa waziri mkuu, chini ya wiki moja kabla ya tarehe ya kutolewa uamuzi wa utawala wa Marekani kuhusu iwapo anastahili kinga ya kutopandishwa kizimbani katika kesi ya mauaji ya mwandishi wa habari, Jamal Khashoggi, kinga ambayo inatolewa kwa wafalme na mawaziri wakuu pekee.

Katika mkondo huo huo gazeti la Guardian la Uingereza limeripoti kuwa, kuteuliwa kwa Muhammad bin Salman kuwa waziri mkuu ni hatua ambayo wataalamu wanasema, itamlinda mwana mfalme huyo kutokana na kesi ya mauaji ya Khashoggi.

Bin Salman, kwa upande mwingine, amewafutilia mbali wapinzani wake wa ndani mmoja baada ya mwingine. Kwa maneno mengine ni kwamba, katika kipindi cha miaka 7 iliyopita, Bin Salman hakubakisha mshindani yeyote mkubwa ndani ya familia ya Al Saud ambaye anaweza kuwa tishio kwa jitihada zake za kukalia kiti cha ufalme wa nchi hiyo.

Katika siku za hivi karibuni pia, kumechapishwa habari kuhusu hali mbaya ya kiafya ya Mohammed bin Nayef, mrithi wa zamani wa mfalme na mpinzani mkuu wa Bin Salman. Ni muda mrefu sasa ambapo Bin Nayef anazuiliwa katika kifungo cha nyumbani.

Bin Salman na Biden

Japokuwa Bin Salman anakosoloewa utokana na mienendo yake isiyofaa na ya kiukandamizaji dhidi ya wanamfalme wenzake wa Saudi Arabia, lakini inatupasa kusema kuwa, ukosoaji huo haujafikia kiwango cha kutishia au hata kuteteresha nafasi yake katika muundo wa madaraka ya nchi hiyo, na hapana shaka kuwa mabadiliko haya mapya ya utawala yanaimarisha zaidi nafasi yake na kumkurubisha zaidi na zaidi katika muradi na lengo lake la kukalia kiti cha ufalme wa Saudia.